Chama tawala nchini Senegal, PASTEF-Les Patriotes, kimechukua hatua ya kumwondoa Rais wa nchi hiyo, Bassirou Diomaye Faye, pamoja na wanachama wengine 31, katika orodha rasmi ya wanachama wake, hatua inayoashiria kuongezeka kwa mgawanyiko kati ya kiongozi huyo na aliyekuwa mshirika wake wa karibu, Ousmane Sonko.
Uamuzi huo ulifikiwa na Baraza la Kitaifa la PASTEF katika kikao chake kilichofanyika Jumanne, Novemba 17, 2026, mjini Dakar, kabla ya kutangazwa rasmi kupitia taarifa ya chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo yenye kumbukumbu namba C N°02/PASTEF/CN/2026, hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia Kifungu cha Sita cha katiba ya chama kinachohusu masharti ya mtu kuendelea kuwa mwanachama.
Baraza hilo lilisema watu 32 waliotajwa katika orodha yake wamepoteza moja kwa moja hadhi ya kuwa wanachama wa PASTEF na hivyo kufutwa kabisa katika orodha rasmi ya wanachama wa chama hicho.
Miongoni mwa waliokumbwa na uamuzi huo ni Rais Faye, ambaye jina lake limeorodheshwa katika nafasi ya saba, pamoja na baadhi ya viongozi waliokuwa na nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya chama.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Faye kuanzisha chama chake cha kisiasa kinachojulikana kama Kiiraay – Les Patriotes républicains, Julai 25, 2026, akionekana kutaka kujenga msingi wake binafsi wa kisiasa nje ya PASTEF.
Kwa mujibu wa katiba ya PASTEF, mtu hupoteza hadhi ya uanachama kwa kujiondoa, kufukuzwa au kujiunga na chama kingine cha kisiasa.
Mvutano kati ya Faye na Sonko umeendelea kuongezeka tangu Mei mwaka huu, wakati Rais huyo alipomwondoa Sonko katika nafasi ya Waziri Mkuu kufuatia kutokubaliana kuhusu namna ya kuendesha serikali na mwelekeo wa utawala.
Sonko, ambaye alikuwa Waziri Mkuu tangu Aprili 2024, baadaye alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Taifa la Senegal, huku akiendelea kuwa kiongozi muhimu ndani ya PASTEF.
Hata hivyo, mgawanyiko huo una mizizi yake katika uchaguzi wa urais wa Machi 2024, wakati Sonko alipomuidhinisha Faye kuwa mgombea wa chama hicho baada ya yeye mwenyewe kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo.
Faye alishinda uchaguzi huo na kumteua Sonko kuwa Waziri Mkuu, hali iliyotafsiriwa kama mwendelezo wa ushirikiano wao wa kisiasa uliokuwa muhimu katika kuiondoa serikali iliyokuwa madarakani.
Lakini uhusiano wao umeendelea kuzorota, huku Sonko akitangaza Novemba 14 kuwa mgawanyiko wake wa kisiasa na Faye hauwezi tena kurekebishwa.
Athari za mgogoro huo zimeanza kuonekana pia bungeni, ambako PASTEF ina wabunge 130 kati ya 165, huku chama kipya cha Faye kikiwa hakina uwakilishi wowote katika Bunge la Taifa.
Hali hiyo imeibua wasiwasi kuhusu uwezo wa serikali kupitisha miswada muhimu, hususan bajeti ya mwaka 2027, pamoja na utekelezaji wa mipango ya kiuchumi wakati nchi hiyo ikikabiliwa na changamoto kubwa za madeni.
Pia kuna wasiwasi kuwa mvutano kati ya makundi hayo unaweza kuathiri ushirikiano wa serikali na Shirika la Fedha Duniani (IMF), hasa katika juhudi za kupata msaada wa kifedha.
Hata hivyo, uamuzi wa PASTEF unahusu uanachama wa chama pekee na haumaanishi kwamba Faye amepoteza mamlaka yake ya urais. Bado anaendelea kuwa Rais wa Senegal kwa mujibu wa nafasi yake ya kikatiba.
Hatua hiyo sasa inaweka wazi zaidi mgawanyiko kati ya viongozi wawili waliokuwa uso wa harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini Senegal, huku mustakabali wa ushirikiano wao ukiendelea kuwa swali kubwa katika siasa za nchi hiyo.









