Wafanyakazi wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waliokuwa wamekwama katika hospitali moja eneo la Akwe, jimbo la Ituri, kwa zaidi ya siku tatu kutokana na mapigano makali, wamefanikiwa kuhamishwa na kufikishwa mahali salama kufuatia juhudi za pamoja za serikali na washirika wa kibinadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amewashukuru wote waliohusika katika operesheni hiyo ya uokoaji, akisema ilitekelezwa katika mazingira magumu kutokana na hali ya usalama iliyokuwa imezorota katika eneo hilo.

Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Dkt. Tedros amesema wafanyakazi wa WHO, Wizara ya Afya ya DRC na wenzao wengine walikuwa wamejisitiri katika hospitali hiyo kwa zaidi ya siku tatu wakikabiliwa na hali tete ya kiusalama.

Amesema kuhamishwa kwao hadi eneo salama kumewezekana kutokana na ushirikiano kati ya sekta ya afya, serikali na mashirika ya kibinadamu yaliyoshirikiana kuhakikisha usalama wao.

Dkt. Tedros ameeleza kushukuru kila mmoja aliyeshiriki katika kufanikisha operesheni hiyo, akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kulinda maisha ya wahudumu wa afya wanaotekeleza majukumu yao katika maeneo yanayokumbwa na migogoro.

Hata hivyo, amesema hali ya usalama inayoendelea kuzorota katika eneo la Mongbwalu imelazimu WHO kuchukua hatua zaidi za tahadhari kwa kuhamisha kwa muda timu yake inayoshughulikia ugonjwa wa Ebola pamoja na washirika wake hadi eneo salama, wakisubiri hali itengemae.

Hatua hiyo inajiri wakati juhudi za kukabiliana na Ebola zikiendelea kuhitaji ushiriki wa wahudumu wa afya, wataalamu na washirika mbalimbali katika maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.

Mongbwalu na maeneo mengine ya jimbo la Ituri yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za kiusalama zinazoweza kuathiri shughuli za kibinadamu, ikiwemo utoaji wa huduma za afya na operesheni za kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

Dkt. Tedros amesisitiza kuwa vituo vya afya, wahudumu wa afya, timu zinazokabiliana na Ebola pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu wanapaswa kulindwa wakati wote, bila kujali ukubwa wa mapigano yanayoendelea.

Amesema usalama wa wahudumu hao ni muhimu ili kuhakikisha wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kuokoa maisha bila kuwekwa katika hatari zinazoweza kuzuilika.

Wito huo unakuja huku mashirika ya afya yakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha migogoro ya kivita haiwi kikwazo kwa upatikanaji wa huduma za matibabu na shughuli za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.