Shehena Ya Mihadarati Ya Sh3.6 Bilioni Yanasa Kwale, Washukiwa Watatu Wakamatwa
Polisi nchini Kenya wamewakamata raia wawili wa Tanzania na mwanamke mmoja raia wa Uganda kufuatia operesheni ya kupambana na biashara ya mihadarati katika Kaunti ya Kwale iliyowezesha kupatikana kwa kilo 454 za dawa inayoshukiwa kuwa Methamphetamine, zenye thamani ya takriban Sh3.6 bilioni katika soko la magendo.
Operesheni hiyo iliongozwa na maafisa wa Shirika la Kitaifa la Kupambana na Dawa za Kulevya (NANB), kutoka eneo la Pwani, kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama vya Kenya na Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, msako huo ulitokana na taarifa za kijasusi zilizowaunganisha washukiwa hao na kukamatwa kwa shehena nyingine ya kilo 259 za dawa zinazoshukiwa kuwa Methamphetamine na Cocaine nchini Tanzania.
Uchunguzi ulipata mwelekeo mpya baada ya mamlaka za Tanzania kumkamata raia mmoja wa nchi hiyo, Saleh Khamis, mwenye umri wa miaka 45, Novemba 5, 2026, kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Khamis baadaye alikabidhiwa kwa maafisa wa polisi wa Kenya katika mpaka wa Lunga Lunga-Horohoro, hatua iliyowezesha kuendelezwa kwa uchunguzi kuhusu mtandao unaoshukiwa kujihusisha na usafirishaji wa mihadarati kuvuka mipaka ya nchi hizo mbili.
Taarifa zilizokusanywa na maafisa wa usalama ziliwaelekeza kwenye operesheni iliyosababisha kupatikana kwa shehena hiyo kubwa ya dawa za kulevya katika Kaunti ya Kwale.
Wakati wa operesheni hiyo, polisi waliwakamata washukiwa hao watatu ambao sasa wanatarajiwa kusaidia katika uchunguzi unaolenga kubaini chanzo cha dawa hizo, zilipokuwa zikisafirishwa na mahali zilipokusudiwa kufikishwa.
Kukamatwa kwa washukiwa hao kunajiri wakati ambapo Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki yanaendelea kukabiliana na changamoto ya mitandao ya kimataifa inayojihusisha na biashara haramu ya mihadarati.
Thamani kubwa ya shehena hiyo pia inaangazia ukubwa wa biashara hiyo haramu na namna inavyoweza kuvuka mipaka ya nchi mbalimbali, huku vyombo vya usalama vikiongeza ushirikiano katika kuwasaka wanaohusika.
Suala la mihadharati limekuwa kikwazo katika baadhi ya mataifa huku walengwa wakubwa wakiwa vijana.









