Kizazi kipya cha uongozi kinaanza kuonekana katika timu ya taifa ya Ureno baada ya kiungo Bernardo Silva kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa kikosi hicho, kufuatia Cristiano Ronaldo kutangaza kustaafu soka la kimataifa.

Silva mwenye umri wa miaka 32, sasa anakuwa sura mpya ya uongozi wa timu hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Ronaldo kwa miaka mingi, huku akipewa jukumu la kuendeleza heshima na ushindani wa Ureno katika medani ya soka duniani.

Kocha Jorge Jesus alithibitisha uteuzi huo wakati akitangaza kikosi cha wachezaji 28 kitakachoshiriki mechi zijazo za Ligi ya Mataifa dhidi ya Denmark na Wales.

Uamuzi huo haukutokana na bahati wala upendeleo, bali mfumo wa Ureno unaotambua uzoefu wa wachezaji kwa kuzingatia idadi ya mechi walizocheza katika timu ya taifa.

Silva ndiye mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi za kimataifa miongoni mwa wachezaji waliopo baada ya Ronaldo, akiwa na jumla ya mechi 115.

Katika orodha ya wachezaji watakaosaidia kubeba jukumu la uongozi, Silva atafuatwa na Rúben Dias, João Cancelo, Rúben Neves na Bruno Fernandes, ambao pia watakuwa sehemu ya kundi la viongozi wa timu hiyo.

SILVA APEWA MZIGO WA KIHISTORIA

Jukumu la Silva si dogo, ikizingatiwa kuwa analirithi kutoka kwa mmoja wa wachezaji walioweka alama kubwa katika historia ya soka la Ureno.

Ronaldo alimaliza safari yake ya kimataifa akiwa na rekodi ya mechi 234 na mabao 146, huku akiongoza Ureno kushinda Euro 2016 na mataji mawili ya Ligi ya Mataifa mwaka 2019 na 2025.

Hata hivyo, Silva si mgeni katika majukumu ya unahodha, kwani amewahi kuvaa kitambaa hicho wakati Ronaldo alipokosekana kikosini.

Kocha Jesus amemsifu kiungo huyo kwa uzoefu, ubora na kiwango chake cha sasa, akisisitiza kuwa ana uwezo wa kuongoza kikosi hicho katika kipindi kipya.

Kwa Silva, nafasi hiyo inakuja wakati muhimu ambapo Ureno inahitaji kuendelea kuwa na ushindani huku ikijenga mustakabali wake bila uwepo wa Ronaldo.

Mashabiki sasa watakuwa na hamuj ya kuona namna atakavyokabiliana na jukumu hilo, hasa katika mashindano makubwa yajayo, ambako Ureno itakuwa ikitafuta kuendeleza mafanikio yake.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwa nahodha mpya ambaye anatarajiwa kuongoza kizazi hicho katika safari ya kuandika ukurasa mwingine wa historia ya soka la Ureno.