Wapenzi wa burudani ya runinga nchini Nigeria na maeneo mbalimbali duniani wameanza kumuomboleza mwigizaji mkongwe wa Nollywood, Pete Edochie, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.
Familia ya mwigizaji huyo ilitangaza kifo chake Jumatano, Novemba 25, 2026, kupitia taarifa iliyosainiwa na mwanawe, Leo Pete Edochie, ikieleza kuwa alifariki saa 6:30 usiku wa manane katika mji wa Enugu nchini Nigeria baada ya kuugua kwa muda mrefu saratani ya tezi dume.
Katika taarifa hiyo yenye kichwa ,An Iroko Has Fallen, familia ilieleza masikitiko yake kufuatia kifo cha mwanamume huyo aliyekuwa mume, baba, ndugu na mmoja wa waigizaji waliotambulika zaidi katika tasnia ya filamu nchini Nigeria.
Familia ilisema mipango ya mazishi yake itatangazwa baadaye, huku ikiwataka mashabiki na watu walioguswa na kifo chake kuiombea familia nguvu na faraja katika kipindi hicho kigumu.
Edochie alizaliwa Machi 7, 1947, katika mji wa Zaria, jimbo la Kaduna, ingawa asili yake ni Akamnato, Ifite Nteje, katika jimbo la Anambra, kusini mashariki mwa Nigeria.
Alianza safari yake ya kikazi katika utangazaji mwaka 1967 alipojiunga na Eastern Nigerian Broadcasting Corporation kama msaidizi wa vipindi. Baadaye alipanda vyeo na kuhudumu katika nafasi za uongozi ikiwemo Mkurugenzi wa Vipindi katika Anambra Broadcasting Service.
Hata hivyo, jina lake lilipata umaarufu mkubwa kupitia uigizaji, hususan baada ya kupewa nafasi ya Okonkwo katika tamthilia ya televisheni ,Things Fall Apart, iliyotokana na riwaya maarufu ya mwandishi Chinua Achebe.
Uigizaji wake wa mhusika huyo ulimjengea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Nigeria, huku akitambulika kwa sauti yake nzito, ufasaha wa mazungumzo na uwezo wa kuigiza wahusika wenye mamlaka katika jamii.
Katika kipindi chake cha miongo kadhaa kwenye tasnia ya filamu, Edochie alishiriki katika kazi mbalimbali zikiwemo ,Igodo, Rituals,Billionaire’s Club, na Lionheart, filamu iliyotayarishwa na mwigizaji na mtayarishaji Genevieve Nnaji mwaka 2018.
Mara nyingi alipewa nafasi za machifu, wafalme, wazee wa familia na viongozi wa jamii, huku matumizi yake ya methali na misemo ya Kiafrika yakimtofautisha na waigizaji wengine.
Mchango wake katika sanaa ulitambuliwa mwaka 2003 alipotunukiwa tuzo ya kitaifa ya Member of the Order of the Niger (MON).
Pia alipokea tuzo ya Industry Merit Award kutoka Africa Magic Viewers' Choice Awards pamoja na tuzo nyingine za kutambua mchango wake katika tasnia ya filamu.
Kifo chake kinaacha pengo katika tasnia ya Nollywood, ambako alihudumu kama mmoja wa waigizaji walioweka msingi wa umaarufu wa filamu za Nigeria na kuhamasisha vizazi vipya vya wasanii.
Edochie ameacha mkewe Josephine Edochie na watoto sita, wakiwemo waigizaji Yul na Linc Edochie.









