Viongozi mbalimbali nchini wameungana kumpongeza Profesa Phoebe Okowa baada ya kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa muhula kamili wa miaka tisa kuanzia 2027 hadi 2036.

Miongoni mwa viongozi waliompongeza ni Rais William Ruto, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, Jaji Mkuu wa sasa Martha Koome na Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing'oei.

Katika ujumbe wake, Martha Koome alisema ushindi wa Okowa ni mafanikio makubwa yanayoonyesha ubora wake katika taaluma ya sheria na kujitolea kwake katika kutetea haki na sheria za kimataifa.

Koome alisema kuchaguliwa kwake ni jambo la kujivunia kwa Kenya na uthibitisho wa imani ambayo jumuiya ya kimataifa imeweka kwa wataalamu wa sheria kutoka nchini.

Alimtakia mafanikio katika kutekeleza majukumu yake mapya, akisema ana imani kuwa atachangia kuimarisha haki za kimataifa, utawala wa sheria na utatuzi wa migogoro kati ya mataifa kwa njia ya amani.

Kwa upande wake, Rais William Ruto alielezea ushindi huo kama wakati wa fahari kubwa kwa Kenya, akisema ni uthibitisho wa utaalamu, uadilifu na ubora wa wataalamu ambao taifa hilo linaendelea kutoa katika masuala ya kimataifa.

Ruto alimtakia Okowa mafanikio katika kutekeleza majukumu yake, akisisitiza umuhimu wa nafasi yake katika kuendeleza sheria za kimataifa na kutafuta suluhu za amani katika migogoro inayohusisha mataifa mbalimbali.

Alihitimisha ujumbe wake kwa kusema Kenya inajivunia mafanikio yake.

Naye aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alielezea ushindi wa Okowa kama uthibitisho mkubwa wa imani ambayo jumuiya ya kimataifa imeweka katika uwezo wake wa kitaaluma na uzoefu wake katika masuala ya sheria.

Maraga alisema ushindi huo unaonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa ina imani na uwezo wa mmoja wa majaji mahiri kutoka Kenya katika kushughulikia masuala ya haki za kimataifa na utawala wa sheria katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutawala.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing'oei, aliushukuru Umoja wa Mataifa na nchi zilizoshiriki katika uchaguzi huo kwa kuunga mkono uteuzi wa Okowa.

Sing'oei pia alizishukuru Sierra Leone, Korea Kusini na Ecuador kwa kuondoa wagombea wao baada ya duru ya tatu ya upigaji kura, akisema hatua hiyo ilisaidia kuzuia uchaguzi huo kuendelea kwa muda mrefu.

Okowa alipata kura 183 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kura 13 katika Baraza la Usalama lenye wajumbe 15, na hivyo kupata ushindi wa kumwezesha kuhudumu kwa muhula kamili.

Atahudumu pamoja na majaji wengine wanne waliochaguliwa kutoka Uingereza, Ufaransa, Jordan na Singapore. Muhula wao mpya utaanza Februari 6, 2027 na kukamilika Februari 5, 2036.

Uchaguzi huo unaimarisha nafasi ya Kenya katika mahakama hiyo yenye makao yake jijini The Hague, Uholanzi, ambayo ina jukumu la kusuluhisha migogoro ya kisheria kati ya mataifa na kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi zilizoidhinishwa za Umoja wa Mataifa.