Uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwaka 2026 nchini Marekani umeibua sura mpya katika historia ya siasa za taifa hilo.

Wagombea kutoka makundi mbalimbali wakivunja rekodi zilizodumu kwa miongo kadhaa na kufungua ukurasa mpya wa uwakilishi katika uongozi wa serikali.

Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne, Novemba 3, yameshuhudia wanawake, Waamerika wenye asili ya Afrika na watu kutoka makundi yaliyokuwa na uwakilishi mdogo katika uongozi wa kitaifa wakipata nafasi muhimu za kisiasa.

Miongoni mwa waliotengeneza historia ni Keisha Lance Bottoms, ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza Mweusi kuchaguliwa kuwa gavana nchini Marekani baada ya kushinda kinyang'anyiro cha ugavana katika jimbo la Georgia.

Ushindi wake pia umeweka alama nyingine ya kisiasa kwa chama cha Democratic, ambacho kimechukua tena usukani wa jimbo hilo baada ya takribani miaka 28 ya utawala wa Republican.

Florida nayo imeandika historia kupitia Byron Donalds, aliyekuwa gavana wa kwanza Mweusi wa Republican kuchaguliwa kuongoza jimbo hilo.

Historia nyingine imeandikwa New Mexico, ambako Deb Haaland amekuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya jamii za wenyeji wa Marekani (Native American) kuchaguliwa kuwa gavana wa jimbo lolote nchini humo.

Haaland aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani katika utawala wa Rais wa zamani Joe Biden, akiwa pia mwanamke wa kwanza kutoka jamii hiyo kushikilia wadhifa huo.

Katika uchaguzi wa kuingia Seneti, Chris Pappas wa chama cha Democratic amekuwa mwanamume wa kwanza aliyejitangaza waziwazi kuwa shoga kuchaguliwa katika Baraza la Seneti la Marekani.

Pappas alishinda kiti cha New Hampshire baada ya kumshinda mpinzani wake wa Republican John E. Sununu.

Minnesota nayo imeshuhudia Peggy Flanagan akiingia katika historia kama mwanamke wa kwanza mwenye asili ya jamii za wenyeji wa Marekani kuchaguliwa kuwa seneta. Ushindi wake umeongeza uwakilishi wa jamii za asili katika taasisi muhimu za kisiasa nchini humo.

Texas imepata gavana wake wa kwanza mwenye asili ya Kilatino kupitia ushindi wa Gina Hinojosa, ambaye pia amemaliza utawala wa Republican katika wadhifa huo uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu.

Aidha, Illinois imeandika historia kupitia Juliana Stratton, ambaye ushindi wake wa kiti cha Seneti umeifanya jimbo hilo kuwa na wanawake wawili wenye asili ya makundi ya watu wa rangi tofauti katika nafasi za uwakilishi wa jimbo hilo katika Seneti.

Mafanikio hayo yanaonyesha mabadiliko katika uwakilishi wa kisiasa nchini Marekani, ambako kwa muda mrefu nafasi nyingi za uongozi zimekuwa zikishikiliwa na makundi machache ya jamii.

Hata hivyo, baadhi ya kinyang'anyiro bado kilikuwa hakijapata mshindi aliyetangazwa rasmi, ikiwemo kile cha Michigan, ambako Abdul El-Sayed alikuwa akiwania kuwa Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa katika Seneti ya Marekani.

Kwa jumla, uchaguzi wa 2026 umeweka alama muhimu katika historia ya demokrasia ya Marekani, huku matokeo yake yakionyesha kuongezeka kwa nafasi za wanawake na makundi mbalimbali ya kijamii katika uongozi wa taifa hilo.