Rais wa Kenya William Ruto amewasili mjini Oyo, nchini Jamhuri ya Congo, kushiriki Mkutano wa Viongozi wa Nchi Nne (Quadripartite Summit) unaowakutanisha Kenya, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Togo.
Mkutano huo unalenga kuwakutanisha viongozi wa nchi hizo kujadili masuala yenye maslahi ya pamoja, yakiwemo ushirikiano wa kikanda, diplomasia, maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo.
Ushiriki wa Rais Ruto katika mkutano huo unaangazia nafasi ya Kenya katika kukuza ushirikiano na mataifa mengine ya Afrika, hasa katika masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya pamoja.
Mkutano huo wa Jumapili, Novemba 22, 2026, umeitishwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Congo Denis Sassou-N’Guesso, huku viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki wakiwa Rais wa DRC Félix Tshisekedi na Rais wa Baraza la Mawaziri la Togo Faure Gnassingbé.
Hata hivyo, mkutano huo unafanyika wakati ambapo uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na DRC umekuwa na changamoto katika miaka ya hivi karibuni, hali inayofanya mazungumzo kati ya Rais Ruto na Tshisekedi kuwa miongoni mwa masuala yanayofuatiliwa kwa karibu.
Mvutano kati ya Nairobi na Kinshasa uliongezeka Desemba 2023 baada ya muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC), unaohusishwa na waasi wa M23, kuzinduliwa jijini Nairobi.
Hatua hiyo iliibua malalamiko kutoka kwa serikali ya DRC, ambayo ilimrejesha nyumbani balozi wake nchini Kenya, ikiishutumu Nairobi kwa kuruhusu kundi hilo kutumia ardhi yake kwa shughuli za kisiasa. Kenya kwa upande wake ilieleza kuwa haiwezi kuzuia uhuru wa kujieleza.
Hali hiyo iliendelea kuathiri uhusiano wa mataifa hayo baada ya Nairobi kuwa mwenyeji wa mikutano iliyohusisha baadhi ya wanasiasa wa upinzani wa Congo, akiwemo rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila, Oktoba 2025.
Ushiriki wa Faure Gnassingbé katika mkutano huo pia una umuhimu wa kidiplomasia kutokana na jukumu lake kama mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo mashariki mwa DRC.
Eneo hilo limekuwa likikabiliwa na mapigano ya muda mrefu kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya Congo, hali iliyosababisha vifo, watu kuyahama makazi yao na kuzidisha changamoto za usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Ingawa ajenda rasmi ya mkutano huo haijawekwa wazi kikamilifu, mazungumzo yanatarajiwa kutoa nafasi kwa viongozi hao kujadili tofauti zao na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Kwa Kenya, mkutano huo unatoa fursa ya kushughulikia masuala yanayoathiri uhusiano wake na DRC, taifa ambalo ni muhimu katika biashara, usalama na ushirikiano wa kiuchumi katika Afrika ya Kati na Mashariki.
Rais Ruto amewasili Congo baada ya kukatiza ziara yake ya maendeleo katika eneo la Magharibi mwa Kenya, iliyoanza Novemba 19, 2026.









