Jeshi la Polisi nchini Tanzania, limewaonya wananchi dhidi ya kujihusisha na makundi yanayodaiwa kuhamasisha vurugu, fujo na vitendo vya kihalifu.
Visa hivyo vinavyotarajiwa kufanyika Novemba 6, 2026, siku ambayo Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anatarajiwa kusomewa hukumu yake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jummane Muliro, amesema jeshi hilo limepokea taarifa kuhusu baadhi ya watu ndani na nje ya Dar es Salaam wanaohamasishana kusafiri kuelekea jijini humo siku hiyo.
Kwa mujibu wa Muliro, baadhi ya watu hao wanadaiwa kuwa na nia ya kufanya fujo na vurugu, hali ambayo imefanya jeshi hilo kutoa tahadhari kwa wananchi na kuwataka kuepuka kushiriki katika mipango inayoweza kuvuruga amani na usalama.
Polisi wamesisitiza kuwa wanatambua haki ya wananchi kufika mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi mbalimbali, ikiwemo ile inayomkabili kiongozi huyo wa CHADEMA.
Jeshi hilo limeeleza kuwa maeneo ya mahakama yanajulikana na yana uwezo wa kuhudumia wananchi wanaohitaji kufika kwa ajili ya shughuli za kisheria, hivyo hakuna sababu ya kuandaa mikusanyiko isiyo rasmi inayoweza kuhatarisha usalama.
Hata hivyo, Muliro amesisitiza kuwa polisi hawatakuwa tayari kuvumilia makundi au watu watakaobainika kupanga, kuhamasisha au kutekeleza vurugu, hujuma na vitendo vingine vya uhalifu kwa kutumia siku hiyo kama fursa.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria, huku akiwataka wananchi kuzingatia taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Tahadhari hiyo inatolewa wakati ambapo kesi ya Tundu Lissu imekuwa ikivuta hisia za kisiasa nchini Tanzania, kutokana na nafasi yake katika CHADEMA na mijadala inayohusiana na mwenendo wa siasa na haki za wananchi.
Siku ya Novemba 6 inatarajiwa kuwa muhimu kwa wafuasi wa chama hicho na wananchi wanaofuatilia kwa karibu kesi hiyo, huku polisi wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu.
Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama, kutoa taarifa kuhusu mipango yoyote ya uhalifu na kuhakikisha kuwa siku hiyo inapita bila matukio yanayoweza kuhatarisha maisha, mali na usalama wa umma.
Polisi wameonya kuwa haki ya kufika mahakamani haipaswi kutumiwa kama kisingizio cha kufanya vurugu au kuvunja sheria.









