Usalama umetiliwa shaka katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyalenda, iliyoko Awasi, Kaunti Ndogo ya Nyando, baada ya wanafunzi wa kidato cha nne kujaribu kuzua ghasia shuleni kufuatia kukamatwa kwa simu mbili za rununu zilizokuwa mikononi mwa baadhi yao.

Tukio hilo lilitokea Jumatatu usiku, Novemba 3, 2026, baada ya wanafunzi hao kukasirishwa na hatua ya walimu kuwanyang'anya simu hizo ambazo ziliripotiwa kupatikana baada ya kukamilika kwa mitihani ya siku hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, hali ilianza kuwa tete baada ya Naibu Mkuu wa Shule kuchukua simu hizo kutoka kwa wanafunzi waliokuwa nazo, hatua iliyowafanya baadhi ya wenzao kuungana na kuanzisha vurugu wakitaka vifaa hivyo virejeshwe.

Inadaiwa kuwa majira ya saa moja usiku, wanafunzi hao walizima taa za shule kabla ya kuvamia ofisi ya Mkuu wa Shule na kuvunja sehemu zake, wakifanikiwa kurejesha simu hizo walizokuwa wamepokonywa.

Hali hiyo ilisababisha taharuki ndani ya shule huku baadhi ya miundombinu ikiharibiwa katika vurugu hizo, ambapo vioo kadhaa vya madirisha vilivunjwa na kuharibika.

Baada ya kupata taarifa kuhusu machafuko hayo, maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Boya walifika shuleni hapo na kuingilia kati ili kurejesha utulivu.

Maafisa hao walifanikiwa kutuliza hali na kuwaamuru wanafunzi kurejea katika mabweni yao ili kuzuia hali hiyo kuendelea kuwa mbaya zaidi.

Katika operesheni hiyo, polisi walifanikiwa kurejesha simu moja pekee kati ya simu mbili zilizokuwa zimechukuliwa na walimu, huku simu nyingine ikiwa bado haijapatikana kufikia wakati wa kuripotiwa kwa tukio hilo.

Licha ya uharibifu wa vioo vya madirisha na uvamizi wa ofisi ya mkuu wa shule, hakuna mwanafunzi aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu usalama na nidhamu katika shule wakati huu ambapo wanafunzi wa kidato cha nne wanaendelea na mitihani yao ya kitaifa ya Cheti cha Elimu ya Sekondari (KCSE).

Aidha, linajiri wakati ambapo shule zinatarajiwa kuhakikisha mazingira salama kwa watahiniwa ili kuwawezesha kukamilisha mitihani yao bila vitisho, vurugu au usumbufu unaoweza kuathiri maandalizi na utulivu wao.

Polisi wanaendelea kufuatilia mazingira yaliyozunguka tukio hilo huku uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo ukiendelea kuibua wasiwasi kuhusu mienendo ya baadhi ya wanafunzi shuleni.