Pete ya almasi iliyokuwa ikivaliwa na mmoja wa manusura maarufu wa ajali ya meli ya Titanic iliyozama mwaka 1912, imeuzwa kwa zaidi ya dola 190,000 za Marekani katika mnada, zaidi ya miaka 114 tangu mkasa huo wa kihistoria utokee.

Pete hiyo iliyokuwa mali ya Lucy Lady Duff Gordon, mmoja wa abiria walionusurika katika ajali hiyo iliyosababisha vifo vya takribani watu 1,500, iliuzwa kwa mnunuzi ambaye utambulisho wake haujawekwa wazi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kuhusu mnada huo, pete hiyo ina almasi iliyokatwa kwa mtindo unaojulikana kama single-cut diamond, huku ikiaminika kuwa ilikuwa zawadi ya uchumba aliyopewa Lady Duff Gordon.

Lady Duff Gordon alikuwa miongoni mwa abiria wa daraja la kwanza waliokuwa ndani ya meli ya Titanic ilipozama katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini baada ya kugonga jiwe kubwa la barafu usiku wa Aprili 14, 1912.

Alikuwa akisafiri pamoja na mumewe, Sir Cosmo Duff Gordon, ambaye pia alinusurika katika mkasa huo uliotikisa dunia na kuwa miongoni mwa majanga makubwa zaidi ya baharini katika historia.

Wawili hao waliokolewa kupitia boti namba moja ya uokoaji, ambayo ilikuwa miongoni mwa boti zilizotumiwa kuwaokoa abiria wakati meli hiyo ilipoanza kuzama.

Hata hivyo, matumizi ya boti hiyo yaliibua utata mkubwa baada ya kuibuka kwa madai kwamba iliondoka ikiwa na nafasi nyingi ambazo zingeweza kutumiwa kuwaokoa abiria wengine waliokuwa wakihangaika kujiokoa.

Pete hiyo iliwasilishwa kwenye mnada na mmoja wa wazao wa moja kwa moja wa familia ya Lady Duff Gordon, ambaye aliamua kuiuza kama sehemu ya urithi wa kifamilia.

Uuzaji wake unaonesha namna vitu vya kihistoria vinavyohusishwa na matukio makubwa duniani vinavyoendelea kuwa na thamani kubwa kwa wakusanyaji wa vitu vya kale na wapenzi wa historia.

Zaidi ya thamani yake ya kifedha, pete hiyo inabeba kumbukumbu ya Lady Duff Gordon na simulizi ya kunusurika katika ajali ya Titanic, tukio ambalo limeendelea kuvutia watafiti, wanahistoria na umma kwa jumla kwa zaidi ya karne moja.

Meli ya Titanic ilizama Aprili 15, 1912, ikiwa katika safari yake ya kwanza kutoka Southampton nchini Uingereza kuelekea New York, Marekani.