Huku joto la kisiasa likizidi kupanda nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wanasiasa wameendelea kuchukua hatua za kimkakati huku kila mmoja akijipanga kuimarisha ushawishi wake na kujihakikishia nafasi katika miungano inayotarajiwa kuibuka.

Miongoni mwa viongozi waliochukua hatua hiyo ni Seneta wa Kisii Richard Onyonka, ambaye amekihama kambi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kujiunga na vuguvugu la kisiasa la Linda Mwananchi.

Onyonka, hata hivyo, amepuuzilia mbali madai kwamba amegeuka dhidi ya Matiang’i, akisema uamuzi wake wa kujiunga na vuguvugu hilo ulifanyika kwa baraka za aliyekuwa waziri huyo.

Matiang’i alikuwa bado hajathibitisha madai hayo kufikia wakati habari hii inaandikwa.

Seneta huyo pia amedokeza kuwa anatarajiwa kuteuliwa kuwa mweka hazina wa vuguvugu hilo, nafasi inayoweza kumpa jukumu muhimu katika kusimamia shughuli zake za kifedha na kuimarisha miundo yake ya kisiasa.

Hatua hiyo inajiri siku chache kabla ya Linda Mwananchi kuzinduliwa rasmi jijini Nairobi siku ya Ijumaa, huku viongozi wanaohusishwa na kundi hilo wakijitayarisha kupanua ushawishi wao kuelekea uchaguzi ujao.

Vuguvugu hilo linahusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na limevutia viongozi kadhaa wanaotaka kuona mwelekeo tofauti wa siasa za upinzani nchini.

Miongoni mwa viongozi wanaohusishwa nalo ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Gavana wa Siaya James Orengo.

Onyonka alikuwa awali amemuunga mkono Sifuna katika azma yake ya kuwania urais, hatua inayoashiria mabadiliko katika misimamo ya kisiasa huku viongozi wakitathmini miungano inayoweza kuimarisha nafasi zao katika uchaguzi wa 2027.

Uamuzi wa seneta huyo pia unaweza kuwa na athari katika siasa za eneo la Gusii, ambako Matiang’i amekuwa akitajwa kama mmoja wa viongozi wanaoweza kuwania urais.

Hata hivyo, Onyonka amesisitiza kuwa kujiunga kwake na Linda Mwananchi hakumaanishi kuwa amevunja uhusiano wake wa kisiasa na Matiang’i.

Wakati huohuo, Linda Mwananchi inatarajiwa kuzindua chama chake cha kisiasa na makao yake makuu jijini Nairobi siku ya Ijumaa kabla ya kufanya mkutano wa kisiasa katika Kaunti ya Kwale siku ya Jumamosi.

Hatua ya Onyonka inaongeza uzito katika mijadala kuhusu mwelekeo wa upinzani na miungano inayoweza kuundwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.