Mahakama Kuu imeamua kuwa matamshi ya Rais William Ruto kuhusu kuwapa walimu na maafisa wa polisi kipaumbele katika ugawaji wa nyumba za bei nafuu hayawezi kutekelezwa kisheria bila msingi katika sheria au sera husika.

Katika uamuzi wake, Jaji Nyaundi Patricia Mande alisema Rais hana mamlaka ya kuweka vigezo vipya vya ugawaji wa nyumba kupitia matamshi ya kiutendaji ikiwa vigezo hivyo havijaainishwa katika sheria zilizopo.

Uamuzi huo unahusu matamshi yaliyotolewa na Rais Juni 3 na Septemba 13, 2025, akipendekeza kuwa asilimia 20 ya nyumba hizo zitengwe kwa walimu na asilimia nyingine 20 kwa maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

Mapendekezo hayo yalipingwa na John Maina Ndegwa na Marshalls Tito Ongoya, waliofikisha ombi la kikatiba mahakamani wakidai kuwa mpango huo ungewapa baadhi ya wafanyakazi manufaa yasiyopatikana kwa Wakenya wengine wanaochangia mpango huo kupitia ushuru wa nyumba za bei nafuu.

Walalamishi walieleza kuwa kutenga jumla ya asilimia 40 ya nyumba hizo kwa makundi hayo mawili kungeibua maswali kuhusu usawa, ubaguzi, upatikanaji wa makazi na matumizi ya fedha za umma.

Walidai pia kuwa hatua hiyo ingewekwa bila kufuata taratibu za kisheria na bila kuhakikisha ushirikishwaji wa umma.

Hata hivyo, upande wa serikali ulitaka kesi hiyo itupiliwe mbali, ukisema kuwa matamshi ya Rais hayakuwa yamebadilisha Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu wala kuondoa mamlaka ya Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu kusimamia ugawaji wa nyumba hizo.

Serikali ilisisitiza kuwa walimu na maafisa wa polisi hawakuwa wamepewa haki ya moja kwa moja ya kupata nyumba hizo kwa kuwanyima waombaji wengine nafasi.

Katika kutupilia mbali hoja hiyo, Jaji Mande alisema kuwa mamlaka ya Rais chini ya Katiba lazima yatumike kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Alibainisha kuwa Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu pamoja na kanuni zake tayari zinaweka mfumo wa ugawaji wa nyumba, hivyo mabadiliko yoyote yanapaswa kufanywa kupitia taratibu zinazotambuliwa kisheria.

Mahakama pia ilisema Wakenya hawapaswi kusubiri haki zao za kikatiba zikiukwe ndipo watafute msaada wa mahakama, ikieleza kuwa wanaweza kuwasilisha kesi pale ambapo kuna tishio la ukiukaji wa Katiba.

Jaji Mande alisisitiza kuwa mamlaka ya kiutendaji yanaweza kusaidia kutekeleza sheria, lakini hayawezi kubadilisha sheria au kuunda upendeleo mpya nje ya mfumo uliowekwa.

Uamuzi huo haujabatilisha Sheria ya Nyumba za "Bei Nafuu" wala kuzuia walimu na maafisa wa polisi kunufaika na mpango huo.

Badala yake, umeweka wazi kuwa upendeleo wowote katika ugawaji wa nyumba lazima uwe na msingi halali wa kisheria au sera inayotambulika.