Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba amewateua Mhariri wa Nation Media Group (NMG) David Muchunguh, Abdirashid Mohamed Hussein na Profesa Joseph Githui Kabiru kuwa wajumbe wa timu ya wadau mbalimbali iliyopewa jukumu la kuchunguza visa vya machafuko na ukosefu wa utulivu katika shule nchini Kenya.
Uteuzi huo umechapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali (Kenya Gazette), ukiwa sehemu ya hatua za serikali kuimarisha juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa ongezeko la visa vya wanafunzi kugoma, kuchoma mabweni na kuharibu mali za shule.
Mbali na wajumbe hao watatu, Ogamba pia amewateua Evelyn Owoko, Catherine Matara, Dkt Fred Odhiambo na Dkt Wilfred Marube kuhudumu kama makatibu wa pamoja wa timu hiyo.
Timu hiyo ina jukumu la kuchunguza chanzo cha machafuko shuleni, kubaini sababu za msingi zinazosababisha wanafunzi kujihusisha na vitendo vya uharibifu pamoja na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha usalama, nidhamu na ustawi wa wanafunzi.
Miongoni mwa masuala yatakayochunguzwa ni ushawishi wa mitandao ya kijamii, matumizi ya simu shuleni, shinikizo la mitihani, uonevu, matumizi ya dawa za kulevya na changamoto za mazingira ya shule za bweni.
Aidha, timu hiyo inatarajiwa kutathmini mifumo ya usalama shuleni, ubora wa huduma za ushauri nasaha, mazingira ya malazi na chakula pamoja na namna walimu na wasimamizi wa shule wanavyoshughulikia malalamishi ya wanafunzi.
Uteuzi huo unajiri kufuatia wimbi la machafuko lililoshuhudiwa katika taasisi mbalimbali za elimu mwaka 2026, ambapo baadhi ya shule zilikumbwa na maandamano, uchomaji wa mabweni na uharibifu wa mali.
Mojawapo ya matukio yaliyotikisa sekta ya elimu ni moto ulioteketeza bweni katika shule ya wasichana ya Utumishi Academy eneo la Gilgil, Kaunti ya Nakuru, Mei 28, 2026, na kusababisha vifo vya wanafunzi 16 huku wengine wakijeruhiwa.
Timu hiyo, inayoongozwa na Profesa Peter Mulwa Mbithi, imepewa siku 90 kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa Waziri wa Elimu, huku ikitarajiwa kutoa taarifa za maendeleo kila mwezi.
Mapendekezo yake yanatarajiwa kusaidia serikali kuweka mikakati mipya ya kuzuia machafuko, kulinda maisha ya wanafunzi na kurejesha utulivu katika taasisi za elimu nchini.









