Ebola Yaua Zaidi 5,000 DRC Huku Maambukizi Yakizidi 10,000
Huku ugonjwa wa Ebola ukiendelea kuwa tishio nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mataifa mengine, mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo umeripotiwa kusababisha vifo vya watu 5,026 nchini DRC, huku jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa ikifikia 10,351 tangu ulipoanza.
Katika ripoti iliyotolewa Jumamosi Novemba 31,2026,Jopo la Rais kuhusu Ebola lilifichua kuwa visa vipya 77 vya maambukizi pamoja na vifo vingine 34 vimeripotiwa, hali inayoashiria kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo bado hayajafikia kikomo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mkoa wa Ituri unaendelea kuwa kitovu cha mlipuko huo, ukichangia asilimia 71 ya visa vyote vilivyothibitishwa nchini humo na asilimia 36.4 ya maambukizi mapya yaliyoripotiwa.
Mlipuko huo umeathiri mikoa minane kati ya mikoa 26 ya DRC, hali inayozua wasiwasi kuhusu uwezekano wa virusi hivyo kusambaa zaidi katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
Takwimu zilizotolewa zinaonesha kuwa wagonjwa 1,101 kwa sasa wanapokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya, huku watu 2,788 wakiripotiwa kupona baada ya kuambukizwa ugonjwa huo.
Hata hivyo, juhudi za kudhibiti Ebola zimeendelea kukabiliwa na vikwazo mbalimbali, huku changamoto za kiusalama katika maeneo ya mashariki mwa DRC zikiathiri shughuli za wahudumu wa afya.
Katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa, timu za kukabiliana na ugonjwa huo zimekumbana na vitisho na mashambulizi kutoka kwa baadhi ya wakazi wanaopinga hatua zinazochukuliwa na mamlaka za afya.
Upinzani huo unatatiza shughuli muhimu za kukabiliana na Ebola, zikiwemo kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa, kuwachunguza wanaoshukiwa kuambukizwa na kuhakikisha walioathirika wanapata matibabu kwa wakati.
Aidha, hali hiyo inazua hofu kwamba kucheleweshwa kwa shughuli za ufuatiliaji na matibabu kunaweza kuongeza hatari ya maambukizi mapya katika jamii.
Mamlaka za afya zinaendelea kukabiliwa na jukumu la kudhibiti mlipuko huo, huku ushirikiano wa wananchi, usalama wa wahudumu wa afya na upatikanaji wa huduma za matibabu vikiwa miongoni mwa mambo muhimu katika juhudi za kukomesha maambukizi.
Kwa sasa,Kenya,DRC na Nigeria ni miongon8 mwa mataifa yaliyoandikisha taarifa kuhusiana na Ebola.









