Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kufuatia kupatikana na hatia ya kupanga na kufadhili mauaji ya mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno, aliyekuwa na ujauzito wa miezi saba wakati wa kifo chake.

Jaji wa Mahakama Kuu Cecilia Wairimu Githua alitoa hukumu hiyo Ijumaa, Novemba 27, 2026, katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi, akieleza kuwa Obado alikuwa mhusika mkuu katika mpango wa uhalifu uliosababisha mauaji ya Sharon mnamo Septemba 2018.

Katika hukumu yake, Jaji Githua alisema Obado ndiye aliyekuwa mbunifu mkuu wa mpango huo wa mauaji, akibainisha kuwa alitoa sababu na fedha zilizotumika kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.

Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi, Michael Juma Oyamo, pia amehukumiwa miaka 25 gerezani, huku aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, Caspal Ajwang Obiero, akihukumiwa miaka 18 jela kutokana na nafasi zao katika mauaji hayo.

Jaji Githua alisema Oyamo alihusika kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa mpango huo, huku Obiero akitoa usaidizi wa vifaa na mipango ya kusaidia kuficha uhalifu huo.

Mahakama ilisema mazingira yaliyoambatana na mauaji hayo yalikuwa mazito zaidi kuliko sababu za kupunguziwa adhabu zilizowasilishwa na washtakiwa hao.

Katika hatua nyingine, jaji alikataa ombi la familia ya Sharon la kutaka Obado apewe adhabu isiyohusisha kifungo gerezani ili aweze kuendelea kusaidia watoto watatu aliowaacha Sharon.

Jaji alisema wajibu wa Obado kuwasaidia watoto hao unapaswa kuendelea hata akiwa gerezani, akionya kuwa mahakama haiwezi kuruhusu watu wanaopatikana na hatia ya makosa mazito kununua uhuru wao kwa kutoa msaada wa kifedha kwa familia za waathiriwa.

Aidha, mahakama ilikataa kutoa amri ya fidia kwa familia ya Sharon, licha ya kutambua maumivu na hasara kubwa waliopitia tangu kifo chake.

Jaji Githua alisema hajaridhishwa kuwa ushahidi wa kutosha kuhusu hasara ya kifedha uliwasilishwa mahakamani ili kuhalalisha malipo ya fidia.

Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, aliuawa Septemba 2018 akiwa na ujauzito wa miezi saba. Mwili wake ulipatikana katika eneo la msitu wa Kodera, Kaunti ya Homa Bay.

Obado, Oyamo na Obiero walipatikana na hatia ya mauaji hayo Julai 23, 2026, baada ya kesi iliyochukua takribani miaka minane kusikilizwa.

Hukumu hiyo inafunga ukurasa muhimu wa kesi iliyotikisa taifa na kuvutia hisia za wengi.