Zimbabwe na Kenya zimekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji wa pande mbili kwa kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru vinavyokwamisha usafirishaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na safari za raia kati ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, amesema makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara yake ya kiserikali nchini Kenya, iliyofanyika kwa mwaliko wa Rais William Ruto, ambapo viongozi hao waliongoza kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Nchi Mbili (Bi-National Commission – BNC).

Katika ujumbe wake baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Mnangagwa amesema mkutano huo umeweka mfumo mpya wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kimkakati kati ya Zimbabwe na Kenya, akisisitiza kuwa mataifa hayo yana historia ya pamoja iliyojengwa wakati wa mapambano ya kudai uhuru.

Amesema chini ya mpango huo, mataifa hayo yameazimia kuongeza biashara na uwekezaji kwa kutumia fursa zinazotolewa na Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) pamoja na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wa mataifa hayo, huku kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara kukilenga kurahisisha bidhaa na huduma kuvuka mipaka bila changamoto zisizo za lazima.

Mbali na biashara, viongozi hao pia wameshuhudia kutiwa saini kwa hati kadhaa za makubaliano na mikataba katika sekta mbalimbali, hatua inayolenga kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.

Mnangagwa amewataka maafisa wa serikali na sekta binafsi katika mataifa yote mawili kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa haraka badala ya kubaki kwenye nyaraka, akisema lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata manufaa halisi kupitia ushirikiano huo.

Katika ziara hiyo, Rais huyo wa Zimbabwe pia ametoa shukrani kwa Kenya na Rais Ruto kwa mchango wao katika kuunga mkono azma ya Zimbabwe kuchaguliwa kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2027–2028.

Aidha, ameishukuru Kenya kwa kuunga mkono Zimbabwe wakati taifa hilo lilipochukua uenyekiti wa COMESA kwa kipindi cha mwaka 2026–2027.

Mnangagwa amesema ushirikiano kati ya Harare na Nairobi una umuhimu mkubwa katika kujenga Afrika yenye uchumi uliounganishwa, utulivu na maendeleo ya pamoja.

Ziara hiyo imehitimishwa huku mataifa hayo yakitarajia kuendeleza ushirikiano kupitia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa, katika hatua inayolenga kuimarisha nafasi ya Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.