Waziri wa Uchukuzi nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa, ameiagiza Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) kumsimamisha kazi nahodha wa meli ya kisasa ya New MV Mwanza, Adam Mwisungu, baada ya uchunguzi kubaini kuwa ajali iliyohusisha chombo hicho katika Ziwa Victoria ilisababishwa na makosa ya kibinadamu.
Agizo hilo limetolewa Alhamisi, Novemba 26, 2026, jijini Mwanza, wakati Profesa Mbarawa akiwasilisha matokeo ya uchunguzi kuhusu ajali iliyotokea Novemba 18, mwaka huu, baada ya meli hiyo kugonga mwamba wa Bismarck wakati wa majaribio ya kiufundi kabla ya kuanza safari zake rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbarawa amesema timu ya uchunguzi ilifanya tathmini ya mazingira ya tukio, kuwahoji wahusika pamoja na kukagua mifumo mbalimbali ya meli hiyo, ikiwemo mifumo ya chumba cha injini, na kubaini kuwa hakukuwa na hitilafu yoyote ya kiufundi iliyochangia ajali hiyo.
Amesema uchunguzi umeonesha kuwa mifumo yote ya meli ilikuwa ikifanya kazi vizuri, hivyo madai yaliyokuwa yakisambaa kwamba ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu za kiufundi hayakuwa na msingi.
Aidha, amekanusha taarifa zilizodai kuwa propela ya meli hiyo ilipinda baada ya kugonga mwamba, akieleza kuwa hali ya meli kuendelea kusafiri kutoka Bandari ya Mwanza Kusini hadi Bandari ya Mwanza Kaskazini inaonesha kuwa madai hayo hayakuwa sahihi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, changamoto kubwa iliyobainika ni namna wahudumu walivyokabiliana na mazingira ya tukio pamoja na kufanya maamuzi kwa wakati, akisisitiza kuwa teknolojia iliyotumika kutengeneza New MV Mwanza inahitaji wataalamu wenye uzoefu na umahiri mkubwa katika uendeshaji wa vyombo vya majini.
Kutokana na matokeo hayo, Serikali imeielekeza TASHICO kuchukua hatua za kinidhamu, kitaalamu na kisheria dhidi ya nahodha huyo pamoja na watumishi wengine watakaobainika kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Vilevile, Serikali imeagiza sehemu ya mbele ya meli iliyoharibika kufanyiwa matengenezo chini ya usimamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), huku mifumo yote ya usalama na uendeshaji ikitakiwa kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuanza kutoa huduma rasmi.
Mkurugenzi Mkuu wa TASHICO, Erick Hamis, amesema meli hiyo ina bima na kwamba tathmini inaendelea kubaini gharama halisi za matengenezo.
Hamis ameeleza kuwa nahodha huyo alikuwa na sifa zinazohitajika kuendesha meli hiyo na kwamba tayari alikuwa ameiongoza katika safari saba za kwenda Bukoba kabla ya ajali hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema nahodha huyo atatakiwa kujiendeleza kitaaluma wakati wa kipindi cha kusimamishwa kazi na kuwasilisha cheti cha mafunzo atakayokamilisha kabla ya kuondolewa zuio hilo.
Katika ajali hiyo, hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, huku mamlaka zikithibitisha kuwa hakuna uchafuzi wa mazingira uliotokea.
New MV Mwanza ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa Serikali katika usafiri wa majini, hivyo Serikali imesisitiza kuwa haitaruhusu meli hiyo kuanza safari rasmi kabla ya kukamilika kwa ukaguzi na kuhakikisha usalama wa abiria, wafanyakazi na mizigo.









