Mchekeshaji maarufu wa Marekani, Shane Gillis, amevunja ukimya kuhusu tuhuma nzito zilizotolewa na aliyekuwa mpenzi wake, Grace Brassel, akichagua kutoa majibu mafupi ya maneno 17 pekee licha ya mwanamke huyo kuchapisha andiko refu lililoeleza madai yake kuhusu uhusiano wao.
Gillis amejibu tuhuma hizo baada ya Brassel kuchapisha makala yenye takribani maneno 3,000 katika jarida maarufu la Marekani la The Cut. Katika andiko hilo, Brassel ameeleza kwa kina changamoto alizodai kukutana nazo wakati wa uhusiano wake wa kimapenzi na mchekeshaji huyo.
Kwa mujibu wa Brassel, wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi uliodumu kwa takribani mwaka mmoja, kipindi ambacho anadai kilikuwa na changamoto mbalimbali zilizomwathiri kihisia na katika maisha yake binafsi.
Miongoni mwa madai aliyoyaibua ni kwamba Gillis alimshinikiza kuacha kazi yake, huku pia akimtuhumu kwa kumsaliti na kumtendea isivyofaa wakati wote walipokuwa pamoja.
Brassel amedai kuwa mazingira ya uhusiano huo yalikuwa magumu na kwamba alikumbana na vitendo ambavyo hakuvitarajia kutoka kwa mtu aliyekuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi.
Aidha, ameeleza kuwa uhusiano wao ulifikia tamati mwezi Agosti mwaka jana, huku akiamua sasa kuweka wazi uzoefu wake kupitia andiko hilo lililozua mjadala kuhusu maisha binafsi ya mchekeshaji huyo.
Hata hivyo, tofauti na andiko refu la aliyekuwa mpenzi wake, Gillis ameamua kutokujibu kila dai lililotolewa dhidi yake, badala yake akitoa kauli fupi iliyolenga kueleza mtazamo wake kuhusu uhusiano huo na kuachana kwao.
Katika majibu yake, Gillis amesema: “Mimi na Grace tulikuwa na nyakati nzuri pamoja. Kuachana ni jambo gumu, na ninamtakia kila la heri.”
Kauli hiyo imekuwa sehemu inayovutia zaidi katika mjadala huo kutokana na namna alivyoweza kujibu tuhuma zilizochukua nafasi kubwa katika andiko la Brassel kwa sentensi chache tu.
Hata hivyo, Gillis hakufafanua zaidi kuhusu madai ya usaliti, shinikizo la kuacha kazi wala madai ya kutendewa vibaya yaliyotolewa na Brassel.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu namna watu maarufu wanavyokabiliana na madai yanayohusu maisha yao ya faragha, hasa pale ambapo aliyekuwa mwenza wao anapoamua kuweka hadharani uzoefu wake wa kimapenzi.
Kwa sasa, Gillis ameishia kutoa salamu za heri kwa aliyekuwa mpenzi wake bila kuingia kwa undani katika madai yaliyotolewa.









