Mwanamume Mkenya Ali Kololo, aliyekaa gerezani kwa zaidi ya muongo mmoja baada ya kuhukumiwa kifo kuhusiana na mauaji ya raia wa Uingereza katika kisiwa cha Lamu, sasa anaituhumu Polisi wa Metropolitan wa London (Met Police) kwa kuharibu maisha yake.

Kololo alihukumiwa mwaka 2013 kufuatia shambulizi lililotokea mwaka 2011 katika nyumba ya mapumziko ya ufukweni iliyokuwa ikikaliwa na wanandoa wa Uingereza, David na Judith Tebbutt.

Katika shambulizi hilo, David alipigwa risasi na kuuawa na watu wenye silaha waliokuwa raia wa Somalia, huku mkewe Judith akitekwa nyara na kupelekwa Somalia ambako alishikiliwa kwa miezi sita.

Maafisa wa Met Police walifika nchini Kenya kusaidia uchunguzi wa tukio hilo, na ushahidi uliotolewa na mmoja wa maafisa hao ukachangia kupatikana kwa hatia kwa Kololo.

Hata hivyo, hukumu yake ilifutwa na Mahakama Kuu ya Kenya Aprili 2023 baada ya kuwepo kwa mashaka kuhusu ushahidi uliotumika kumtia hatiani.

Katika mahojiano yake ya kwanza na BBC, Kololo amesema kukamatwa, kuteswa na kufungwa kwa muda mrefu kulimnyang'anya maisha aliyokuwa nayo, huku familia yake ikivunjika.

Kabla ya kukamatwa, Kololo alikuwa akifanya kazi ya kukata miti na kuuza kuni ili kuitunza familia yake iliyokuwa na mke na watoto watatu.

Anasema baada ya kukamatwa ndani ya saa 24 tangu kutokea kwa shambulizi hilo, alipigwa na kuteswa na polisi wa Kenya ili kulazimishwa kukiri kuhusika na tukio hilo.

Kololo anadai kuwa hakuweza kusoma wala kuandika na alilazimishwa kuweka alama ya kidole kwenye taarifa aliyodai hakuelewa yaliyokuwa yameandikwa.

Mwaka 2023, uchunguzi wa Ofisi Huru ya Malalamiko dhidi ya Polisi nchini Uingereza (IOPC) ulibaini kuwa aliyekuwa afisa wa Met Police, Neil Hibberd, aliacha kuwasilisha mahakamani ushahidi muhimu wa kisayansi ambao ungeweza kuathiri kesi hiyo.

IOPC ilisema Hibberd angekuwa na kesi ya kujibu kuhusu utovu mkubwa wa nidhamu, lakini hakuweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuwa alikuwa tayari amestaafu.

Kololo sasa anaishtaki Met Police, akitaka fidia kwa madai ya ushahidi wa kupotosha na hatua zisizokuwa halali zilizochangia kuhukumiwa kwake. Polisi hao wanapinga madai hayo mahakamani.

Met Police imesema haiwezi kutoa maoni kuhusu madai ya Kololo, lakini imesema inaendelea kujitolea kusaidia mamlaka za Kenya kupata haki kwa familia ya Tebbutt.

Kololo anasema licha ya kupata uhuru, bado anaugua kutokana na mateso aliyopitia, hana uwezo wa kufanya kazi ya kukata miti na amepoteza uhusiano wa karibu na watoto wake.

Amesema hata akipata fidia kubwa, maisha yake hayatakuwa kama zamani, lakini fedha hizo zingemsaidia kujitunza na kusaidia watoto wake.