Mwanamuziki maarufu wa Marekani Kanye West na mkewe Bianca Censori wanaripotiwa kupanga kufanya upya hafla ya kufunga ndoa yao, katika hatua inayoweza kuwa mwanzo wa ukurasa mpya wa uhusiano wao.

Habari hizo zimeibuka kupitia mmoja wa wanafamilia wa Censori, aliyefichua kuwa wawili hao wana mpango wa kufanya upya viapo vya ndoa, miaka kadhaa baada ya kufunga ndoa kwa mara ya kwanza.

Taarifa hiyo imezua gumzo miongoni mwa mashabiki wa wawili hao, hasa kutokana na historia ya uhusiano wao ambao umekuwa ukivutia hisia za watu kutokana na matukio mbalimbali yanayohusisha maisha yao binafsi na mwonekano wao hadharani.

Kanye, ambaye pia anajulikana kama Ye, ni mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa hip-hop duniani, huku Bianca akiwa mbunifu wa majengo kutoka Australia ambaye amekuwa akitajwa sana kwenye vyombo vya habari tangu uhusiano wake na mwanamuziki huyo ulipojulikana.

Wawili hao walifunga ndoa Januari 2023, muda mfupi baada ya Kanye kukamilisha taratibu za talaka na aliyekuwa mkewe, nyota wa vipindi vya televisheni Kim Kardashian.

tangu wakati huo, ndoa yao imekuwa ikizungumziwa sana, huku safari zao katika miji mbalimbali, mavazi ya Bianca na kuonekana kwao pamoja kwenye matukio ya burudani vikichochea mijadala kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na TMZ, mipango hiyo imefichuliwa na shangazi yake Bianca, Kelly, ambaye alizungumza kupitia kipindi cha redio cha Australia cha Fifi, Fev & Nick.

Kelly aliwaambia watangazaji kuwa ndugu kadhaa wa familia ya Censori wanajiandaa kusafiri kutoka Australia kwenda Marekani mwezi Desemba kuhudhuria sherehe hiyo.

Akizungumzia maandalizi hayo, Kelly alifafanua kuwa Kanye na Bianca tayari ni mume na mke, lakini wanapanga kubadilishana viapo vya ndoa kwa mara nyingine.

Hata hivyo, katika simulizi lililowachekesha watangazaji wa kipindi hicho, Kelly alifichua kuwa licha ya kuwa sehemu ya familia, yeye mwenyewe hakualikwa kwenye sherehe hiyo.

Wanandoa hao walifunga ndoa kwa siri Desemba 20, 2022, katika sherehe iliyofanyika Palo Alto, California, Marekani, muda mfupi baada ya Kanye kukamilisha talaka yake na Kim Kardashian.

Kanye na Kim walikuwa wameoana mwaka 2014 na kupata watoto wanne ambao ni North, Saint, Chicago na Psalm kabla ya ndoa yao kuvunjika.

Uhusiano wa Kanye na Bianca umeendelea kuwa gumzo duniani, hasa kutokana na mitindo ya mavazi ya Bianca ambayo mara kadhaa imeibua mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwaka 2025, kulikuwa na taarifa za uwezekano wa wawili hao kutengana kufuatia misukosuko iliyohusishwa na kauli na matendo ya Kanye, lakini baadaye walionekana kurejesha uhusiano wao na kuendelea kuonekana pamoja hadharani.

Kwa sasa, taarifa za kuhuisha viapo vya ndoa zinaashiria hatua nyingine katika safari yao ya kimapenzi, ingawa wawili hao bado hawajatoa uthibitisho rasmi kuhusu sherehe hiyo.

Pia, madai ya kuwepo kwa kadi ya mwaliko iliyotajwa kwenye mitandao ya kijamii yamehusisha Desemba 20, 2026, kama tarehe inayoweza kutumika kwa hafla hiyo, ingawa maelezo hayo hayajathibitishwa.

Iwapo mipango hiyo itatekelezwa, Kanye na Bianca watakuwa wakitumia maadhimisho ya miaka minne tangu ndoa yao ya siri kuipa safari yao ya ndoa sura mpya.

Na kwa mashabiki wao, swali kubwa sasa ni moja: Je, safari hii kutakuwa na sherehe kubwa ya kifahari au Kanye ataamua tena kufanya mambo kwa mtindo wake wa kipekee?Nso swali