Mfanyabiashara na mwanasiasa Suleiman Shahbal ameitaka Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwekeza katika klabu ya Mombasa United, akisema kupandishwa kwa timu hiyo hadi Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ni fursa muhimu ya kukuza soka na kutangaza kaunti hiyo.

Shahbal alisema timu hiyo inahitaji usaidizi wa wadau mbalimbali ili kuimarisha ushindani wake katika ligi kuu, huku akiwahimiza viongozi wa kaunti kuweka kando tofauti zao na kuunga mkono maendeleo ya soka la eneo la Pwani.

Akizungumza na wanahabari katika uwanja wa Serani, Mombasa, wakati wa uzinduzi wa toleo la pili la mashindano ya Shahbal Super Cup, mfanyabiashara huyo pia alikanusha madai kwamba amejiondoa katika ufadhili wa Mombasa United.

Alisisitiza kuwa bado amejitolea kusaidia klabu hiyo ambayo alisema aliisaidia kukua kutoka ngazi za chini hadi kufikia ligi kuu nchini.
“Tulianza Mombasa United kutoka ngazi za chini hadi Ligi Kuu, na hilo ndilo lilikuwa lengo letu.Kwa nini niondoke sasa? Hii ni timu yangu, ni timu yetu, na Anza Fresh ameijenga. Taarifa kwamba nimejiondoa katika ufadhili si za kweli,” alisema Shahbal.

Kauli yake inajiri baada ya rais wa klabu hiyo, Abdirahman Hussein, maarufu kama Anza Fresh, na Afisa Mkuu Mtendaji Nick Arunga kuashiria kuwa uongozi ulikuwa ukitafuta wafadhili wengine kufuatia taarifa za uwezekano wa Shahbal kusitisha ufadhili wake.

Hata hivyo, Shahbal alisema uhusiano wake na uongozi wa klabu hiyo uko imara na kwamba juhudi za kutafuta ufadhili zaidi zinaendelea.

Alifichua kuwa yeye na Anza Fresh walikutana na mwenyekiti wa kampuni ya SportPesa jijini Dubai, ambapo waliahidiwa msaada kwa timu hiyo. Aliongeza kuwa mazungumzo na kampuni ya Azam yanaendelea kwa matumaini ya kupata ufadhili zaidi.

Shahbal pia aliwakosoa wanasiasa aliowatuhumu kuingiza siasa katika masuala ya klabu hiyo, akiwataka kuiacha timu ijikite katika malengo yake ya soka.

Alisema baadhi ya wanasiasa wameanza kujihusisha na timu hiyo baada ya kupata umaarufu, licha ya kutokuwa mstari wa mbele ilipokuwa ikikabiliana na changamoto za kupanda ngazi.

Wakati huo huo, toleo la pili la Shahbal Super Cup linatarajiwa kuanza mwezi Novemba, huku timu zikishindana kuanzia ngazi ya wadi. Bingwa wa kaunti atazawadiwa shilingi milioni moja pamoja na zawadi nyingine.

Shahbal alisema mashindano hayo yanalenga kukuza vipaji vya vijana na kuibua klabu nyingine kutoka Mombasa itakayoweza kucheza ligi kuu.

Alipendekeza timu hiyo mpya iitwe Mombasa City, akisema ana matumaini ya kuona kaunti hiyo ikiwasilishwa na klabu mbili katika ligi kuu, kwa mfano wa Manchester City na Manchester United nchini Uingereza.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa FKF Mombasa, Alamin Ahmed Abdalla, alisema mashindano hayo yatasaidia kuinua viwango vya soka katika eneo la Pwani na kutoa fursa kwa klabu zaidi kupanda hadi Ligi Kuu ya Kenya.