Mwimbaji na mwigizaji maarufu wa Marekani, Jennifer Lopez, amezua mjadala mitandaoni baada ya kudai kuwa tasnia ya filamu ya Hollywood haijampa nafasi inayostahili kutokana na kutokuwa mzungu, kauli iliyochochea ukosoaji kutoka kwa mashabiki, wachambuzi na watu mbalimbali mashuhuri.

Katika mahojiano na vyimbo vya habari, nyota huyo mwenye asili ya Kilatino alisema kuwa wakurugenzi wa filamu na watu wanaohusika na upangaji wa waigizaji bado wana vigezo fulani vya mwonekano wanavyovipa kipaumbele wanapotafuta wasanii wa kuwashirikisha katika filamu.

Lopez alieleza kuwa hali hiyo imemlazimu kujitengenezea nafasi yake mwenyewe katika tasnia ya burudani ili kuendelea kujenga jina lake kama msanii mwenye asili ya Kilatino.

Hata hivyo, kauli hiyo haikupokelewa vizuri na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao walipinga madai yake, wakieleza kuwa mwigizaji huyo amekuwa na mafanikio makubwa Hollywood kwa miongo kadhaa na ameshiriki katika takribani filamu 44.

Wakosoaji hao walitumia historia yake ya uigizaji na nafasi mbalimbali alizowahi kupata katika filamu kubwa kuhoji madai kwamba Hollywood imempuuza kwa sababu ya rangi ya ngozi yake.

Miongoni mwa waliomkosoa ni Adrianne Curry-Rhode, aliyewahi kushiriki katika kipindi cha utafutaji wanamitindo cha America’s Next Top Model, ambaye alitumia kauli kali kuelezea madai ya Lopez akiyataja kuwa ni kujidanganya kupita kiasi.

Kwa upande wake, mtangazaji wa Fox News, Tomi Lahren, pia alijiunga na wakosoaji hao kwa kutoa maoni mafupi ya kejeli akisema, "LOL, sure Jan", kauli inayotumiwa kuonyesha kutokuamini jambo linalosemwa.

Lopez, ambaye amejijengea umaarufu kupitia muziki na filamu, amekuwa miongoni mwa mastaa wanaotambulika kimataifa kutokana na kazi zake katika tasnia hizo mbili.

Miongoni mwa filamu alizowahi kuigiza ni The Wedding Planner na Shotgun Wedding, ambazo zilimsaidia kuendeleza umaarufu wake kama mwigizaji wa Hollywood.

Hata hivyo, mjadala unaoendelea unaibua tena suala la uwakilishi wa watu wenye asili tofauti katika tasnia ya filamu ya Marekani, hasa kuhusu nafasi wanazopewa waigizaji kutoka jamii za wachache.

Hadi sasa, mjadala huo unaendelea kusambaa mitandaoni huku baadhi ya watu wakiunga mkono hoja ya Lopez kuhusu changamoto za waigizaji wa Kilatino, na wengine wakitilia shaka madai yake kutokana na mafanikio aliyoyapata katika kipindi chote cha kazi yake.