Mahakama Kuu nchini Kenya imewaamuru maafisa wakuu wa polisi kumfikisha mwanaharakati wa upinzani kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, mbele yake akiwa hai au amefariki, huku maswali yakiibuka kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwake.

Jaji Alexander Muteti ametoa agizo hilo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ruai, akiwataka kumwasilisha Mwaipaya mahakamani Jumatatu, Novemba 2, 2026, saa tano asubuhi.

Maafisa hao pia wameamriwa kuwasilisha hati halisi ya kumzuilia Mwaipaya na kueleza sababu zinazofanya aendelee kushikiliwa, pamoja na kwa nini asiamriwe kuachiliwa mara moja.

Agizo hilo limetolewa baada ya shirika la Vocal Africa kuwasilisha ombi la dharura mahakamani Oktoba 27, 2026, kwa niaba ya mwanaharakati huyo.

Jaji Muteti alitangaza ombi hilo kuwa la dharura na kuwataka Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja Kirocho, pamoja na mkurugenzi wa DCI, Amin Mohamed Ibrahim, kufika mahakamani wao wenyewe au kupitia mawakili wao kueleza mazingira ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa Mwaipaya.

Waliohusishwa katika kesi hiyo wamepewa hadi Jumatatu saa tatu asubuhi kuwasilisha na kuwafikishia wahusika wengine majibu yao. Kesi hiyo itatajwa tena saa tano asubuhi kwa maelekezo zaidi ya mahakama.

Mzozo huo unaibua upya wasiwasi kuhusu usalama wa wanaharakati na madai ya utekaji nyara katika eneo la Afrika Mashariki, ambako visa vya watu kutoweka na madai ya kukamatwa bila maelezo ya wazi vimeendelea kuzua mjadala.

Nchini Kenya, madai ya kutoweka kwa watu, wakiwemo wanaharakati na wakosoaji wa serikali, yamekuwa yakizua maandamano na wito wa kutaka vyombo vya usalama viwajibishwe. Familia za baadhi ya waliotoweka zimekuwa zikidai kufahamu walipo wapendwa wao, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitaka uchunguzi wa kina.

Nchini Tanzania, madai ya kukamatwa na kutoweka kwa baadhi ya wakosoaji wa serikali pia yamekuwa yakizua wasiwasi kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kisiasa.

Visa hivyo vimeongeza wito wa kutaka mataifa ya Afrika Mashariki yaheshimu haki za binadamu na kuhakikisha kuwa watu wanaokimbilia nchi jirani kutafuta usalama hawakabiliwi na vitisho au kurejeshwa kwa nguvu katika nchi walizokimbia.

Miongoni mwa visa vilivyozua mjadala ni kutoweka kwa mwanasiasa wa upinzani wa Uganda, Dkt. Kizza Besigye, jijini Nairobi mnamo Novemba 2024, kabla ya kuibuka Uganda ambako alikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai pia aliripotiwa kutekwa Nairobi Januari 2025, lakini akaachiliwa baadaye siku hiyo.

Uamuzi wa Jumatatu unatarajiwa kutoa mwanga zaidi kuhusu aliko Mwaipaya na hatua zilizochukuliwa na mamlaka za Kenya kufuatia kutoweka kwake.