Bingwa wa zamani wa mbio za Boston Marathon, Sharon Jemutai Cherop, ameanzisha hatua za kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Eldoret uliompa mumewe wa zamani, Mathew Bowen, asilimia 40 ya mali zinazozozaniwa na wawili hao zenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Cherop amesema hajaridhishwa na uamuzi huo na amemwagiza wakili wake kuelekea katika Mahakama ya Rufaa ili kupinga hukumu hiyo, akisisitiza kuwa mali hizo zilinunuliwa kwa fedha alizopata kutokana na kushiriki mashindano mbalimbali ya riadha ya kimataifa.
Mzozo huo unahusu mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya takriban shilingi milioni 40, zikiwemo nyumba za makazi, majengo ya kupangisha na mashamba yaliyoko katika kaunti za Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet.
Katika stakabadhi alizowasilisha mahakamani, Cherop alieleza kuwa alitumia mapato yake kutokana na mashindano ya kimataifa kujenga utajiri huo wakati alipokuwa akishiriki riadha kwa kiwango cha juu.
Alitaja mapato ya mashindano mbalimbali aliyoshiriki, yakiwemo Boston, Hamburg, Toronto na Turin, pamoja na mikataba ya kibiashara iliyochangia mapato yake.
Kwa upande wake, Bowen amedai kuwa alichangia katika upatikanaji na uendelezaji wa mali hizo, akisema alihusika katika shughuli za ununuzi na ujenzi wa baadhi ya majengo yanayozozaniwa.
Bowen, ambaye pia ni mwanariadha wa zamani na baadaye akawa meneja na mpiga mwendo wa Cherop katika mazoezi na mashindano, amesisitiza kuwa anastahili sehemu ya mali hizo kutokana na mchango wake wakati wa ndoa yao.
Mzozo huo umeibuka baada ya ndoa yao kuvunjika rasmi, huku pande zote mbili zikitoa madai tofauti kuhusu mchango wao katika kujenga utajiri wa familia.
Historia ya Boston Marathon
Cherop aliandika historia katika ulimwengu wa riadha mwaka 2012 aliposhinda mbio za Boston Marathon nchini Marekani, mojawapo ya mashindano maarufu na ya kihistoria zaidi ya mbio ndefu duniani.
Mbio hizo zilianza mwaka 1897, zikiwa zimechochewa na mafanikio ya mbio za marathon katika Michezo ya Olimpiki ya kisasa ya mwaka 1896. Mashindano hayo hufanyika kila mwaka katika eneo la Boston, jimbo la Massachusetts, na ni miongoni mwa mashindano mashuhuri zaidi katika kalenda ya kimataifa ya riadha.
Cherop alitwaa taji la wanawake mwaka 2012 baada ya kumaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2 dakika 31 na sekunde 50. Mwaka mmoja kabla ya ushindi huo, alikuwa amemaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo hayo.
Mbali na mafanikio yake Boston, Cherop pia alijizolea medali ya shaba katika mbio za marathon kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2011 jijini Daegu, Korea Kusini.
Hata hivyo, wakati mafanikio yake ya riadha yalimwezesha kujenga mali kutokana na zawadi za mashindano na mikataba ya kibiashara, sasa anakabiliwa na mzozo wa kisheria kuhusu umiliki na mgawanyo wa utajiri huo.
Hatua yake ya kukata rufaa inafungua ukurasa mwingine wa mzozo huo, huku uamuzi wa mwisho kuhusu mgawanyo wa mali ukisubiriwa katika hatua zinazofuata za kesi.









