Kiongozi wa Democratic Party of Kenya (DP) na mmoja wa viongozi wa upinzani, Justin Muturi, amekosoa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kile alichokitaja kuwa uzembe katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, akisema tume hiyo haiwezi kulaumu kesi za mahakamani huku yenyewe ikishindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati.
Muturi amesema ingawa kesi za kisheria zinazohusu ununuzi wa teknolojia ya uchaguzi zinaweza kuchelewesha baadhi ya shughuli za maandalizi, mwenendo wa tume hiyo pia unachangia kuhatarisha maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Katika taarifa yake, kiongozi huyo wa upinzani amesema IEBC inapaswa kuwajibika kwa ucheleweshaji wa hatua muhimu za maandalizi badala ya kuelekeza lawama kwa mahakama, akisisitiza kuwa Wakenya wanahitaji tume inayochukua jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uaminifu.
Amedai kuwa tume hiyo tayari iko nyuma katika utekelezaji wa baadhi ya hatua muhimu zinazohitajika katika mpango wa maandalizi ya uchaguzi, hali inayopaswa kushughulikiwa kwa haraka ili kuepusha changamoto zaidi kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia.
Aidha, Muturi ameelezea wasiwasi wake kuhusu madai kuwa maafisa wakuu wa IEBC, akiwemo Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) na mkuu wa kitengo cha ununuzi, wako nje ya nchi kwa shughuli ambazo zingeweza kuahirishwa kutokana na umuhimu wa majukumu yao katika kipindi hiki.
Amesema maafisa hao wana nafasi muhimu katika mchakato wa kutangaza mshindi wa zabuni ya teknolojia itakayotumika katika uchaguzi wa 2027, hivyo kutokuwepo kwao wakati huu kunazua maswali kuhusu vipaumbele vya tume hiyo.
Vilevile, Muturi amedai kuwa mchakato wa zabuni hiyo umesimamishwa ili kuruhusu baadhi ya wajumbe wa kamati ya tathmini kusafiri nje ya nchi, hatua aliyosema inaashiria kutokuwepo kwa hali ya dharura katika kushughulikia suala hilo.
Amesema IEBC haiwezi kuitaka mahakama kuharakisha usikilizaji wa kesi zinazohusu zabuni hiyo huku yenyewe ikisimamisha shughuli zake kwa sababu ya safari za nje ya nchi.
Kuhusu gharama za ununuzi wa teknolojia hiyo, Muturi amesisitiza kuwa fedha za umma hazipaswi kutumiwa kwa gharama zilizopandishwa, akidai kuwa baadhi ya kampuni zenye sifa zinazotambulika ziliwasilisha zabuni zilizokuwa ndani ya bajeti iliyoidhinishwa.
Ameonya kuwa endapo mkataba utatolewa kwa gharama zinazozidi bajeti licha ya kuwepo kwa wazabuni waliokidhi masharti ndani ya kiwango kilichotengwa, hatua hiyo itachukuliwa kama matumizi mabaya ya fedha za walipa ushuru.
Kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo wa DP ameitaka IEBC kuwarejesha mara moja maafisa wote muhimu wanaohusika na mchakato wa ununuzi, kuendeleza tathmini ya zabuni bila kuchelewa zaidi na kuhakikisha mchakato mzima unafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma ya mwaka 2015.
Muturi amesema Wakenya wanafuatilia kwa karibu mwenendo wa maandalizi hayo na kwamba maafisa wote waliopewa jukumu la kusimamia uchaguzi watawajibika kwa maamuzi na hatua zao.









