Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewaagiza maafisa wa usalama kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wanasiasa wanaochochea ghasia kwa kutumia tofauti za kikabila na kisiasa, akionya kuwa serikali haitavumilia viongozi wanaochochea chuki miongoni mwa Wakenya.
Murkomen amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanasiasa wanaotumia majukwaa ya kisiasa kuwagawanya wananchi kwa misingi ya ukabila au kuchochea jamii mbalimbali kupigana.
Akizungumza Jumapili, Novemba 22, 2026, katika ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo eneo la Marioshoni, Molo, Kaunti ya Nakuru, Murkomen alitoa maagizo hayo kwa makamishna wa kaunti na makamanda wa polisi kuhakikisha kuwa wanaotekeleza vitendo hivyo wanachukuliwa hatua.
Waziri huyo alisema hakuna kiongozi atakayesamehewa kutokana na wadhifa wake, iwe ni mwanasiasa anayewania kiti cha kisiasa kwa mara ya kwanza au kiongozi ambaye tayari anahudumu katika ofisi ya umma.
Alisisitiza kuwa siasa za Kenya hazipaswi kugeuzwa uwanja wa kuchochea uhasama kati ya jamii, akionya kuwa viongozi wanaotumia tofauti za kikabila kujipatia uungwaji mkono wanahatarisha amani na mshikamano wa taifa.
Murkomen alisema serikali haitakubali siasa zinazowageuza wananchi kuwa maadui kwa misingi ya jamii wanazotoka, akitaka ushindani wa kisiasa kujikita katika sera na ajenda za maendeleo.
Onyo hilo linajiri wakati shughuli za kisiasa zikianza kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027, huku viongozi mbalimbali wakianza kujiweka katika nafasi za kisiasa na kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wananchi.
Aidha, Murkomen alizungumzia visa vya baadhi ya watu kuvamia mashamba ya wakazi wa Marioshoni na kuvuna viazi bila idhini ya wamiliki, akisema vitendo hivyo havitavumiliwa.
Alidai kuwa baadhi ya wanaohusika katika uvamizi huo wamekuwa wakitumia majina ya watu wenye ushawishi kujihalalishia vitendo vyao, jambo alilosema ni kinyume cha sheria.
Aliwaonya wote wanaoingia katika mashamba ya watu na kuvuna mazao bila ruhusa kuwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Waziri huyo aliongeza kuwa serikali haitaruhusu watu wachache kuvuruga uhusiano mwema uliopo baina ya wakazi wa eneo hilo kupitia vitendo vya uhalifu.
Murkomen amekuwa akisisitiza umuhimu wa kudumisha usalama nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao, akiwataka viongozi wa kisiasa kutanguliza amani na kuepuka kauli zinazoweza kusababisha machafuko.









