Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, amewataka viongozi wa upinzani kujiepusha na matamshi na vitendo vinavyoweza kuchochea machafuko nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu, 2027.

Murkomen amesema serikali imeweka kipaumbele suala la amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha kuvuruga usalama wa wananchi.

Waziri huyo aliyasema hayo alipohudhuria hafla ya Amaya Youth Empowerment Initiative katika viwanja vya Amaya Plesian, eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo, baada ya kufanya ziara ya kutathmini hali ya usalama katika eneo hilo.

Katika hotuba yake kwa wakazi, Murkomen aliipongeza jamii ya eneo hilo kwa kuendelea kudumisha mshikamano na kuishi kwa amani, akiwataka kuendeleza utamaduni huo licha ya changamoto mbalimbali zinazolikabili eneo hilo.

Hata hivyo, alielekeza sehemu ya hotuba yake kwa masuala ya kisiasa nchini, ambapo alikosoa hatua ya viongozi wa upinzani kujiondoa katika mkutano wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akisema hatua hiyo haikuwa na sababu za msingi.

Murkomen aliwashutumu viongozi hao kwa kutumia masuala ya uchaguzi kuibua mvutano wa kisiasa, akidai kuwa wanapaswa kuheshimu taasisi za kikatiba badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuongeza mgawanyiko nchini.

Aidha, alimuonya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye kwa sasa ni kinara wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), dhidi ya wito wa kuandaa maandamano nchini, akisisitiza kuwa masuala yanayohusu uchaguzi na utangazaji wa matokeo ya urais yanaongozwa na katiba.

Alisema kuwa utaratibu wa kutangaza matokeo ya uchaguzi umewekwa wazi kikatiba na viongozi wote wanapaswa kuheshimu sheria pamoja na taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia mchakato huo.

Waziri huyo pia alidai kuwa baadhi ya viongozi wa upinzani wanaonyesha dalili za wasiwasi kuhusu uchaguzi ujao, akiwataka kuelekeza nguvu zao katika shughuli za kisiasa zinazozingatia sheria.

Katika hatua nyingine, Murkomen aliwahakikishia vijana na wananchi wanaotarajia kushiriki zoezi lijalo la kuajiri maafisa wa polisi kuwa mchakato huo utakuwa huru na wa haki.

Aliwataka waombaji kujitokeza kwa wingi bila hofu ya kubaguliwa au kulazimika kutoa fedha ili kupata nafasi, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya rushwa katika zoezi hilo.

Murkomen alisema serikali itaendelea kushirikiana na jamii katika kuimarisha usalama na kuhakikisha nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 ikiwa na amani na utulivu.