Familia moja katika Kaunti ya Bomet imekumbwa na majonzi baada ya mwanamume mmoja kudaiwa kuwaua watoto wake wawili kwa kuwachoma kisu kifuani kabla ya kujaribu kujitoa uhai kwa kunywa sumu, tukio lililotokea wakati mkewe akiwa mbali akishiriki shughuli za kusahihisha mitihani.

Mshukiwa huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Nicholas Cheruiyot, mwenye umri wa miaka 32, alikamatwa Jumapili, Novemba 22, 2026, baada ya kuokolewa na maafisa wa polisi kutoka kwa umati wa wananchi waliokuwa wametaka kumshambulia kufuatia tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Morongo, eneo la Chambori, Kaunti Ndogo ya Bomet Mashariki, ambapo watoto hao wenye umri wa miaka saba na minne walidaiwa kushambuliwa kwa kisu kifuani.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Bomet, Joel Chebii, alisema mshukiwa alijaribu kujiua kwa kutumia sumu baada ya kuwashambulia watoto hao.

Cheruiyot alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Longisa kwa matibabu, huku polisi wakisema atafunguliwa mashtaka mawili ya mauaji pamoja na jaribio la kujiua baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Majirani walieleza kuwa tukio hilo huenda lilichochewa na mzozo wa kifamilia kati ya mshukiwa na mkewe, ambaye anafanya kazi ya ualimu.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwanamume huyo alikuwa amewahi kutoa vitisho vya kufanya jambo baya na baadaye kujitoa uhai, ingawa hawakutarajia kuwa angehusisha watoto wake katika tukio hilo.

Mmoja wa majirani, Beatrice Chepkirui, alisema walisikia watoto wakilia kwa uchungu kutoka ndani ya nyumba na kuanza kushuku kuwa walikuwa wakishambuliwa.

Alisema walijaribu kumshawishi baba huyo asiwadhuru watoto na kumtaka atafute msaada wa kutatua matatizo yake ya kifamilia, lakini juhudi zao hazikufua dafu.

Baadaye majirani walilazimika kuvunja mlango wa nyumba hiyo ili kuwaokoa watoto, lakini walipofika ndani waliwakuta tayari wamejeruhiwa vibaya na kuvuja damu nyingi.

Mshukiwa pia alipatikana akiwa amedhoofika baada ya kudaiwa kunywa sumu, huku akiwa na kisu kinachoshukiwa kutumika katika mauaji hayo.

Polisi wameanzisha uchunguzi kubaini mazingira kamili yaliyopelekea tukio hilo, huku miili ya watoto hao ikitarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Tukio hilo limezua maswali kuhusu kuongezeka kwa visa vya vurugu za kifamilia na athari zake kwa watoto wasio na hatia.