Polisi katika eneo la Emuhaya, kaunti ya Vihiga, wameanzisha uchunguzi kuhusu visa vitatu tofauti vya utekaji nyara vilivyoripotiwa katika maeneo ya West Bunyore na North East Bunyore, huku miili ya watu wawili waliotekwa ikipatikana katika Mto Yala.

Kati ya visa hivyo vitatu, viwili viliripotiwa West Bunyore huku kisa kingine kikitokea North East Bunyore.

Hata hivyo, mtu mmoja aliyetambuliwa kama Wilson Mukuna wa Ebukholi, Esibuye, bado hajapatikana, hali inayozua wasiwasi miongoni mwa familia yake na wakazi wa eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Emuhaya, George Opere Ongozi, amethibitisha kuwa mmoja wa watu waliotekwa nyara ni afisa wa polisi Manase Olambwe Ndakala, aliyetoka eneo la Emusire.

Ongozi amesema mshukiwa mmoja tayari amekamatwa kuhusiana na visa hivyo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira ya utekaji nyara na vifo vya waathiriwa hao.

Kamanda huyo aliyasema hayo alipofanya ziara nyumbani kwa marehemu Ndakala katika eneo la Ebuyangu, ambapo pia alikutana na familia yake na kutoa pole kufuatia kifo cha afisa huyo.

Aidha, aliahidi kuwa serikali itagharamia mazishi ya marehemu kwa mujibu wa kanuni na taratibu za huduma ya polisi.

Hata hivyo, kuhusu aliko Wilson Mukuna, Ongozi amesema maafisa wa usalama wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichomtokea na kumtafuta.

Wakati huohuo, familia ya Ndakala, ikiongozwa na mama yake mzazi Florida Ndakala, imesema imekumbwa na changamoto kubwa za kifedha wakati wa juhudi za kutafuta na kupata mwili wa jamaa yao katika Mto Yala.

Familia hiyo imeomba msaada wa kifedha kukabiliana na gharama zilizojitokeza, ikieleza kuwa marehemu ameacha watoto wawili wadogo ambao sasa wamepoteza mzazi wao.

Katika eneo la Esibuye, wakazi waliandamana kulalamikia kutoweka kwa Wilson Mukuna, wakitaka serikali kuingilia kati na kuongeza juhudi za kumtafuta.

Wakazi hao wamesisitiza kuwa familia ya Mukuna inahitaji majibu kuhusu aliko mpendwa wao, huku wakitaka uchunguzi wa haraka ili kubaini waliohusika na visa hivyo.

Visa hivyo vitatu vimeibua hofu kuhusu usalama wa wakazi wa Emuhaya, huku jamii ikisubiri hatua zaidi za polisi na kupatikana kwa Mukuna.