Kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ameendelea kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya baada yaĵ kuwapokea wajumbe kutoka Kaunti ya Nyeri na Ukambani katika makazi yake ya Wamunyoro.
Ziara hiyo inajiri wakati ambapo aliyekuwa Naibu Rais akiendeleza mikutano na mashauriano na viongozi mbalimbali katika juhudi za kuimarisha upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.
Pamoja na wajumbe wengine,Gachagua amewapokea Charity Ngilu,Wavinya Ndeti na wajumbe webgine, lengo likiwa ni kuandaa mikakati kabambe kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kinara huyo wa DCP amekuwa akitumia makazi yake ya Wamunyoro kama kitovu cha mikutano ya kisiasa, huku akijaribu kujenga ushirikiano na viongozi kutoka maeneo tofauti nchini.
Hivi majuzi, Gachagua alikutana na viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, katika mkutano uliozua matumaini ya ushirikiano mpana ndani ya upinzani.
Wakati wa mazungumzo hayo, Gachagua alisisitiza umuhimu wa viongozi kushirikiana akisema, “I want us to be together. We are one team, and we mean well for the country.”
Aidha, alikataa madai kwamba ushirikiano wake wa kisiasa na viongozi wengine unasukumwa na ukabila, akitaja uamuzi wake wa kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2022 licha ya kutoka jamii tofauti.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na Inooro TV, Gachagua pia alizungumzia uwezekano wa kuunda muungano unaowahusisha yeye, Sifuna na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, akimtaja pia Eugene Wamalwa katika hesabu zake za kisiasa.
Alidai kuwa ushirikiano wa viongozi hao ungeunda nguvu kubwa ya kisiasa inayoweza kukabiliana na Ruto katika uchaguzi ujao.
Gachagua hata amewahi kueleza kuwa yuko tayari kumuunga mkono Sifuna kama mgombea urais na hata kuwa mgombea mwenza iwapo viongozi wa upinzani watakubaliana kuhusu mpangilio huo.
Hata hivyo, mipango hiyo ya kuunganisha upinzani imekumbwa na mvutano kuhusu uongozi na nafasi za viongozi katika serikali ijayo.
Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, hivi karibuni alidai kuwa Gachagua alitaka mgao wa asilimia 50 wa serikali katika mazungumzo na viongozi wa Linda Mwananchi, madai ambayo yameibua maswali kuhusu mazungumzo ya kugawana mamlaka.
Gachagua sasa anaendelea na mikutano yake ya kisiasa huku akitafuta kuimarisha uungwaji mkono wake katika Mlima Kenya na maeneo mengine, wakati viongozi wa upinzani wakijaribu kufikia makubaliano ya pamoja kabla ya uchaguzi wa 2027.









