Baada Ya Miaka 28: Mwingereza Akamilisha Safari Ya Kuzunguka Dunia Kwa Miguu
Ndoto ya kutembea kuzunguka dunia kwa miguu imekamilika baada ya miaka 28 na siku moja, huku raia wa Uingereza, Karl Bushby, mwenye umri wa miaka 57, akirejea nyumbani katika mji wa Hull, Uingereza, Novemba 2, 2026.
Bushby alirejea nyumbani baada ya kukamilisha safari ndefu aliyoipa jina la Goliath Expedition, aliyoianzisha Novemba 1, 1998, nchini Chile akiwa na umri wa miaka 29.
Alipoanza safari hiyo, Bushby alijiwekea masharti magumu mawili ambayo aliyazingatia kwa kipindi chote cha safari yake. Kwanza, aliamua kutotumia usafiri wa mitambo kumsaidia kusonga mbele, huku sharti la pili likiwa kutorejea nyumbani hadi atakapokamilisha azma yake ya kuzunguka dunia kwa miguu.
Katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili, Bushby amepitia maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo Amerika ya Kati, Marekani, Canada, Urusi, Asia ya Kati na sehemu mbalimbali za Ulaya.
Hata hivyo, safari hiyo haikuwa ya kawaida kwani ilimlazimu kukabiliana na changamoto nyingi, zikiwemo magonjwa, migogoro ya kivita, vikwazo vya kupata visa na mazingira hatarishi yaliyotishia usalama wake.
Miongoni mwa hatua zilizovutia zaidi katika safari yake ni kuvuka Bahari ya Bering, pamoja na kuogelea kwa siku 31 katika Bahari ya Caspian, juhudi zilizoongeza ugumu wa safari hiyo ya kihistoria.
Kwa mujibu wa makadirio, Bushby amesafiri takribani kilomita 75,000 tangu alipoanza safari yake nchini Chile mwaka 1998.
Akizungumza baada ya kuwasili nyumbani, Bushby ameeleza kuwa mafanikio hayo hayakuwa juhudi zake pekee, bali yalichangiwa pia na msaada wa watu mbalimbali aliokutana nao katika maeneo tofauti duniani.
Aidha, amewahimiza watu kutambua uwezo wao, kuamini ndoto zao na kutokata tamaa wanapokumbana na changamoto katika safari ya kutimiza malengo yao.
Kurejea kwake nyumbani kunahitimisha safari iliyoanza akiwa na umri wa miaka 29 na kukamilika akiwa na miaka 57, ikiwa ni ushahidi wa muda, uvumilivu na kujitolea katika kutimiza azma aliyojiwekea.
Hii kwake imekuwa ni hatua kubwa ya kutimiza hitaji la moyo wake na wanaomzunguka









