Polisi nchini Zimbabwe wamethibitisha kukamatwa kwa Mchungaji Uebert Angel, ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Rais Emmerson Mnangagwa na Balozi wa Kimataifa, akikabiliwa na tuhuma za udhalilishaji wa kingono na kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo, Kamishna Paul Nyathi, amesema Angel alikamatwa mchana wa Jumapili, Novemba 23, 2026, huku akithibitisha kuwa uchunguzi kuhusu tuhuma hizo unaendelea.

"Tunathibitisha kukamatwa kwa Nabii Uebert Angel mchana huu kuhusiana na tuhuma za udhalilishaji wa kingono na kufanya mapenzi kinyume na maumbile," alisema Nyathi, akiongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Harare, mchungaji huyo alikamatwa wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa lake lililopo eneo la Hippodrome, Braeside, ambalo pia ni makao makuu ya huduma yake ya kidini.

Hata hivyo, polisi hawajafafanua kwa kina mazingira ya tuhuma zinazomkabili wala kueleza ni lini atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo.

Kukamatwa kwake kunafuatia taarifa iliyochapishwa na gazeti moja nchini Zimbabwe mwezi Machi mwaka huu, iliyodai kuwa mwanamke mmoja alikuwa amewasilisha malalamiko akidai kufanyiwa udhalilishaji wa kingono katika kanisa hilo.

Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo kukamatwa kwa Angel kunahusiana moja kwa moja na malalamiko hayo.

Tukio hilo pia linajiri wiki chache baada ya mchungaji huyo kujitokeza hadharani kumuunga mkono Makamu wa Rais Constantino Chiwenga wakati wa mvutano wa kisiasa ndani ya chama tawala cha Zanu PF kuhusu suala la urithi wa uongozi.

Siku chache baadaye, Angel alitangaza tena uaminifu wake kwa Rais Mnangagwa, hatua iliyozua mijadala miongoni mwa wachambuzi na watoa maoni nchini humo.

Baadhi ya wachambuzi nchini Zimbabwe wamehusisha muda wa kukamatwa kwake na mvutano huo wa kisiasa, ingawa polisi hawajatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.

Angel ni mhubiri na mfanyabiashara anayefahamika katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kutokana na huduma zake za kidini na wafuasi wake wengi, wakiwemo wa nchini Zambia.

Kwa sasa, tuhuma zinazomkabili bado hazijathibitishwa mahakamani na anachukuliwa kuwa hana hatia hadi pale itakapothibitishwa vinginevyo kwa mujibu wa sheria.

Polisi wamesema watatoa taarifa zaidi kuhusu kesi hiyo kadri uchunguzi utakavyoendelea.