Serikali ya Korea Kusini imesisitiza kuwa uwepo wa wanajeshi wake katika Ghuba ya Aden haupaswi kutafsiriwa kama hatua ya kujiunga na vita vinavyoendelea dhidi ya Iran, ikieleza kuwa dhamira yake ni kulinda raia wake, meli za kibiashara na maslahi ya kiuchumi ya taifa hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini, Kang Shin-chul, amesema mpango wa kupanua shughuli za kikosi cha wanamaji cha Cheonghae katika eneo hilo haumaanishi kuwa Seoul inashiriki moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mzozo wa kijeshi unaohusisha Iran.

Akizungumza mbele ya wabunge, Kang amesema kikosi hicho kinaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda usafiri wa majini na kukabiliana na uharamia, badala ya kushiriki operesheni za kijeshi dhidi ya taifa lolote.

Amesema hatua ya kuimarisha shughuli za kikosi hicho imechochewa na ongezeko la matukio ya uharamia katika eneo hilo, huku akibainisha kuwa visa hivyo vimeongezeka mara tatu ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kikosi cha Cheonghae kimekuwa kikifanya doria katika Ghuba ya Aden tangu mwaka 2009, kikilenga kulinda meli za Korea Kusini pamoja na kuhakikisha usalama wa raia wake wanaotumia njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji.

Hatua ya Seoul inajiri wakati mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran ukiendelea kuathiri usalama wa njia muhimu za usafirishaji wa mafuta na bidhaa katika Mashariki ya Kati.

Korea Kusini inategemea kwa kiasi kikubwa uagizaji wa mafuta kutoka eneo hilo, hali inayofanya usalama wa njia za majini kuwa suala muhimu kwa uchumi wake.

Serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la Marekani kuhusu uwezekano wa kutoa msaada wa kijeshi katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Hata hivyo, Rais wa Korea Kusini Lee Jae-myung amekuwa akisisitiza kuwa nchi yake haitatuma wanajeshi kushiriki vita dhidi ya Iran wala kuchukua hatua zitakazoifanya kuwa sehemu ya mzozo huo.

Lee amesema serikali yake itaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda meli za kibiashara, njia za usafirishaji wa mafuta na usalama wa raia wake.

Kwa mujibu wa serikali ya Korea Kusini, shughuli za kikosi cha Cheonghae zitakuwa za kujilinda na kulinda usafiri wa majini, huku kikosi hicho kikiendelea kufanya kazi kwa kujitegemea bila kujiunga na majeshi ya mataifa yanayohusika katika vita hivyo.