Viongozi wa dini mbalimbali katika Kaunti ya Kisumu wamewataka wanasiasa kuacha kutumia vijana kufanya vurugu za kisiasa, wakionya kuwa hali ya kutovumiliana kisiasa na kuajiri makundi ya wahuni inaweza kuhatarisha usalama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Viongozi hao, wanaowakilisha madhehebu ya Kikristo, Kiislamu, Kihindu na jumuiya nyingine za kidini, wamesema wana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya vitisho, uchochezi, misimamo mikali ya kisiasa na mashambulizi yanayohusishwa na ushindani wa kisiasa katika kaunti hiyo.
Katika taarifa ya pamoja iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kisumu Interfaith, Askofu Betty Onyango, pamoja na makamu wake Ali Zakaria, viongozi hao wametaka wanasiasa kuhakikisha michakato ya mchujo wa wagombea ndani ya vyama vya kisiasa inafanyika kwa amani, haki na uwazi.
Wamesisitiza kuwa uchaguzi wa mchujo unaotarajiwa kufanyika kati ya Februari na Machi 2027 unapaswa kuamuliwa kupitia kura na hoja za wagombea badala ya vitisho, mawe, mashambulizi na vitendo vya kuwazuia wapinzani kufanya kampeni.
"Tunalaani vikali kuajiri vijana kama wahuni wa kisiasa, kutovumiliana kisiasa, kuanzishwa kwa maeneo ambayo baadhi ya wagombea hawawezi kufika, pamoja na matamshi ya chuki na uchochezi katika mitandao ya kijamii na mikutano ya kisiasa," sehemu ya taarifa hiyo imesema.
Viongozi hao pia wameelezea wasiwasi kuhusu hali ya usalama katika Kaunti ya Kisumu, wakitaja ongezeko la visa vya uporaji, mashambulizi ya kimwili na kingono pamoja na ujambazi wa kutumia silaha.
Wamezitaka idara za usalama kuwakamata si wahusika wa moja kwa moja pekee, bali pia watu wanaowapanga na kuwafadhili kufanya vurugu, wakisisitiza kuwa wanaofadhili vitendo hivyo wanapaswa kuwajibishwa.
Aidha, wameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) pamoja na vyombo vya usalama kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wanasiasa wanaojihusisha na ununuzi wa kura.
Wamesema vitendo vya kuwapa wapiga kura fedha, chakula, pombe, ajira, bursari na zawadi nyingine kwa lengo la kuwashawishi kuwapigia kura wagombea fulani vinadhalilisha wapiga kura na kudhoofisha demokrasia.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wametangaza utayari wao wa kutumia makanisa, misikiti na mahekalu kama maeneo ya upatanishi kati ya wagombea wanaokinzana, wafuasi wa vyama tofauti na makundi ya vijana ili kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa ghasia.
Pia wamewataka wazazi, walezi na taasisi za kidini kuhakikisha watoto wanashiriki shughuli zenye manufaa wakati wa likizo ndefu ili kuwalinda dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, pombe, unyanyasaji wa kingono na misimamo mikali ya kisiasa.
Viongozi hao wametangaza mpango wa kuimarisha vilabu vya amani kwenye shule, vyuo na jamii, huku wakifichua kuwa mashindano ya kitaifa ya mijadala ya Amani Clubs mwaka ujao yataandaliwa katika Shule ya Upili ya Maseno.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa pamoja ulioungwa mkono na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Baraza la Makanisa na Dini mbalimbali nchini (IRCK), kwa ushirikiano na NCIC pamoja na Utawala wa Serikali za Kitaifa (NGAO).
Wamehitimisha kwa kuwataka Wakenya kushirikiana kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2027 unafanyika bila ghasia, wakisisitiza kuwa hakuna kiti cha uongozi kinachostahili kumwaga damu.









