Muswada wa sheria unaopendekeza kubadilisha mfumo wa malipo ya huduma za intaneti nchini Kenya umezua mjadala mkali kuhusu faragha ya watumiaji, uwezekano wa ufuatiliaji wa shughuli zao mtandaoni pamoja na ongezeko la gharama za kupata huduma hiyo.
Muswada huo unaojulikana kama Kenya Information and Communications (Amendment) Bill, 2025, unaodhaminiwa na Mbunge wa Aldai Marianne Jebet Kitany, unapendekeza kampuni zinazotoa huduma za intaneti kufuatilia kiasi cha data kinachotumiwa na kila mteja na kuwatoza kulingana na matumizi yao halisi.
Chini ya mapendekezo hayo, kila mtumiaji atapewa nambari maalumu ya utambulisho wa matumizi ya intaneti, huku kampuni zikihitajika kufuatilia matumizi hayo, kuyaweka katika mfumo unaoeleweka na kutoa bili kulingana na kiwango cha data kilichotumika.
Wanaounga mkono muswada huo wanasema hatua hiyo inalenga kuwalinda watumiaji dhidi ya kutozwa fedha zisizoendana na huduma wanazopokea.
Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA), kampuni za mawasiliano na mashirika ya kutetea haki za binadamu zimeibua maswali kuhusu umuhimu wa kuifanya mifumo hiyo kuwa ya lazima na namna taarifa binafsi za watumiaji zitakavyolindwa.
Tume ya Kimataifa ya Wanasheria nchini Kenya (ICJ Kenya) imehoji umuhimu wa kukusanya taarifa zinazoweza kumtambulisha mtumiaji kupitia matumizi yake ya intaneti, ikisema mamlaka zilizopo tayari zina uwezo wa kushughulikia malalamiko ya bili na kulinda watumiaji.
Wakosoaji wanataka kuwe na maelezo ya wazi kuhusu nani ataruhusiwa kupata taarifa hizo, zitahifadhiwa kwa muda gani na mazingira yatakayoruhusu kushirikishwa kwa watu au taasisi nyingine.
Wasiwasi huo unaibuka wakati Kenya ikiendelea kujadili masuala ya faragha ya kidijitali, hasa baada ya kesi iliyomhusu mwanafunzi wa chuo kikuu David Ooga Mokaya, aliyewahi kukamatwa kutokana na chapisho lake mitandaoni kuhusu Rais William Ruto.
Mokaya aliachiliwa huru Februari mwaka huu baada ya mahakama kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi yake. Baadaye aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu akilalamikia namna taarifa zake binafsi za mawasiliano zilivyoshughulikiwa.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Mawasiliano imependekeza badala ya kulazimisha mfumo mpya wa malipo, kampuni zitoe tahadhari kwa wateja wanapofikia asilimia 50, 80 na 100 ya vifurushi vyao vya data.
Pia imependekeza kuwepo kwa mifumo ya kuangalia matumizi ya data kwa wakati halisi na kuweka ukomo wa matumizi ya fedha kila mwezi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Telkom Kenya, Mugo Kibati, ameonya kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuongeza gharama za kampuni na kudhoofisha uwekezaji katika sekta ya intaneti.
Amesema takribani asilimia 96 ya usajili wa huduma za data nchini unahusisha intaneti ya simu, ambayo tayari hutozwa kulingana na kiasi cha data kinachotumiwa.
Muswada huo sasa unachunguzwa na Kamati ya Bunge kuhusu Mawasiliano, Habari na Ubunifu huku wabunge wakikabiliwa na jukumu la kusawazisha ulinzi wa watumiaji, gharama za intaneti na haki ya wananchi ya faragha.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, mjadala huo unazidi kuangazia umuhimu wa kuhakikisha sheria mpya hazizuii upatikanaji wa intaneti kwa gharama nafuu wala kudhoofisha haki za kidijitali









