Waziri wa Elimu nchini Kenya, Julius Migos Ogamba, amewaonya wanafunzi wanaoshiriki katika vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani ya kitaifa ya Cheti cha Elimu ya Sekondari (KCSE), akisema serikali haitasita kufutilia mbali matokeo ya watakaopatikana na makosa hayo.
Onyo hilo linajiri wakati mtihani wa KCSE wa mwaka huu ukiwa umeandamwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo taarifa za baadhi ya wanafunzi kujifungua wakati wa kipindi cha mitihani, wengine kufariki dunia na visa vya vurugu vilivyoripotiwa katika baadhi ya vituo.
Aidha, kumekuwa na matukio ya kutisha yanayohusisha usalama wa wasimamizi wa mitihani, huku baadhi ya wanafunzi wakiripotiwa kuwashambulia wasimamizi na hata katika tukio jingine kumpokonya polisi silaha.
Akizungumza katika ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Sosiot (DCC), baada ya kusimamia usambazaji wa karatasi ya mwisho ya mtihani wa KCSE, Ogamba alisema serikali itachukua hatua kali dhidi ya watahiniwa watakaohusika katika ukiukaji wa kanuni za mitihani.
Alisema hatua hizo zitawahusu pia wanafunzi watakaoshambulia wasimamizi wa mitihani au maafisa wengine waliopewa jukumu la kuhakikisha zoezi hilo linaendeshwa kwa utaratibu.
Ogamba alisisitiza kuwa matokeo ya watahiniwa watakaopatikana wakijihusisha na udanganyifu au vurugu yanaweza kufutiliwa mbali, akiwataka wanafunzi kuheshimu kanuni na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao wa elimu.
Waziri huyo pia aliwahakikishia watahiniwa, wazazi na walimu kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kuendelea na masomo bila kujali alama atakazopata katika mtihani huo.
Alisema serikali inatambua kuwa matokeo ya mitihani siyo mwisho wa safari ya elimu, akibainisha kuwa mifumo iliyopo inalenga kuwasaidia wanafunzi kuendelea na hatua nyingine za masomo na mafunzo.
Katika hatua nyingine, Ogamba aliahidi kuwa serikali itahakikisha fedha za uendeshaji wa shule, maarufu kama capitation, zinatolewa mapema ili kuimarisha shughuli za taasisi za elimu.
Alisema kiwango cha fedha hizo kinahitaji kufanyiwa mapitio kwa kuwa viwango vinavyotumika kwa sasa viliwekwa mwaka 2015 na hivyo vinahitaji kuangaliwa upya kulingana na hali ya sasa ya kiuchumi.
Alieleza kuwa timu maalumu itaundwa kuanza mchakato wa kutathmini upya kiwango hicho, akiongeza kuwa serikali inalenga kuhakikisha shule zinapata rasilimali zinazohitajika kutoa elimu bora.
Matamshi ya Ogamba yanakuja wakati wadau wa elimu wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kulinda usalama wa watahiniwa, wasimamizi na maafisa wengine wanaohusika na mitihani ya kitaifa.









