Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, amefichua kuwa Ikulu ya Rais nchini humo imekuwa ikiathiriwa na changamoto za upatikanaji wa maji na umeme, hali inayokumba mamilioni ya wananchi wanaokabiliwa na huduma duni za msingi.

Tinubu alisema changamoto hiyo imefikia hadi katika makazi yake rasmi ya Aso Rock yaliyoko jijini Abuja, akisimulia jinsi alivyokumbwa na ukosefu wa maji wakati akijinyoa wiki iliyopita.

Akizungumza Jumapili, Novemba 22, 2026, katika ibada maalumu ya maombi iliyoandaliwa na familia yake katika klabu ya Yoruba Tennis jijini Lagos, kiongozi huyo alisema maji yalikoma kutoka ghafla alipokuwa akijinyoa Jumatano iliyotangulia.

Alisema tukio hilo limemfanya kutambua kwa namna ya moja kwa moja changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma muhimu, licha ya kuwa anaishi katika makazi rasmi ya Rais.

"Jumatano ya wiki iliyopita nilikuwa najinyoa, lakini maji yakakoma kutoka. Hata Ikulu kuna changamoto hizo," alisema Tinubu, akielezea hali iliyozua vicheko miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.

Rais huyo alikiri kuwa ukosefu wa maji na umeme ni miongoni mwa changamoto kubwa za miundombinu zinazoendelea kuathiri maendeleo ya Nigeria, akiahidi kuwa serikali yake itachukua hatua kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa.

Alisisitiza kuwa upatikanaji wa umeme na maji ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, akisema nchi haiwezi kupiga hatua ikiwa huduma hizo hazipatikani kwa uhakika.

"Hakuna mwanga, hakuna maji, hakuna umeme, hakuna maendeleo. Tumeanza tu na tunaweza kurekebisha changamoto hizi kwa ajili ya Nigeria," alisema.

Nigeria, ambayo ni taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, imekuwa ikikabiliwa na changamoto za muda mrefu katika sekta ya nishati, huku kukatika kwa umeme kukilazimu baadhi ya kaya na biashara kutegemea jenereta na vyanzo vingine vya nishati.

Wakati huohuo, upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Kauli ya Tinubu imeibua mjadala kuhusu hali ya huduma za msingi nchini humo, hasa baada ya kufichua kuwa hata makazi ya kiongozi mkuu wa taifa hayaepukani na changamoto hizo.

Katika mkutano huo, Tinubu pia alitumia fursa hiyo kuwataka wafuasi wa chama chake cha All Progressives Congress (APC) kuimarisha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Aliwataka viongozi wa chama hicho kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuungana katika juhudi za kuwahamasisha wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo.