Mchezo maarufu wa Grand Theft Auto 6 (GTA 6) umevunja rekodi za mauzo katika tasnia ya burudani duniani, baada ya kukadiriwa kuingiza zaidi ya dola bilioni 2.3 (takribani Shilingi bilioni 304) kufuatia uzinduzi wake uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa kwa miaka 13.
Takwimu zilizotolewa na kampuni ya uchambuzi wa soko la michezo ya video, Sensor Tower, zinaonyesha kuwa GTA 6 ilikuwa imeuza zaidi ya nakala milioni 24.5 kufikia Alhamisi, Novemba 19, siku ambayo mchezo huo ulizinduliwa rasmi.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, mchezo huo umeingiza takribani dola bilioni 2.36, sawa na pauni bilioni 1.8, na hivyo kuibuka miongoni mwa uzinduzi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya burudani.
Mafanikio hayo yanaashiria ukubwa wa soko la michezo ya video duniani, ambalo limeendelea kukua na kushindana na sekta nyingine za burudani ikiwemo filamu, muziki na televisheni.
Kwa kulinganisha, filamu iliyofanya vizuri zaidi katika mapato ya sinema mwaka huu, Spider-Man: Brand New Day, imeingiza takribani dola bilioni 2.5 katika kipindi chote ilichoonyeshwa kwenye majumba ya sinema.
Hata hivyo, kampuni ya Rockstar Games inayotengeneza GTA 6 pamoja na kampuni mama ya Take-Two Interactive bado hazijatoa takwimu rasmi za mauzo ya mchezo huo, ingawa zimesema mahitaji kutoka kwa wateja yamekuwa makubwa yasiyo ya kawaida.
GTA 6 ni mwendelezo wa mfululizo wa michezo ya Grand Theft Auto ulioanza karibu miongo mitatu iliyopita na ambao umejijengea umaarufu mkubwa kutokana na mazingira yake ya wazi yanayowaruhusu wachezaji kuchunguza miji, kuendesha magari na kushiriki katika matukio mbalimbali.
Toleo jipya linaangazia wahusika wawili wakuu, Lucia na mwenzi wake Jason, wanaoishi katika jimbo la kubuniwa la Leonida, ambalo limechochewa na jimbo la Florida nchini Marekani.
Mchezo huo umefanyiwa kazi kwa muda mrefu huku uzinduzi wake ukiahirishwa mara kadhaa, jambo lililoongeza hamu miongoni mwa mashabiki duniani.
Sensor Tower imesema umaarufu wa GTA 6 unatarajiwa pia kupunguza muda ambao wachezaji watatumia katika michezo mingine ya aina moja kwa takribani asilimia 10.
Takwimu zake zinatokana na uchambuzi wa risiti za manunuzi ya kidijitali na taarifa kutoka kwa mamilioni ya watumiaji wa majukwaa mbalimbali ya michezo.
GTA 6 inapatikana kupitia PlayStation 5 na Xbox Series X/S, huku mafanikio yake ya awali yakionyesha nguvu kubwa ya biashara ya michezo ya video katika soko la kimataifa.









