Kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ameipa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) hadi Januari mwaka ujao kushughulikia malalamishi ya upinzani kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027, akionya kuwa maandamano ya nchi nzima yataandaliwa iwapo madai hayo hayatashughulikiwa.

Gachagua amesema upinzani hautasita kuhamasisha Wakenya kuandamana endapo tume hiyo itashindwa kuchukua hatua kuhusu masuala ambayo wanayaona kuwa muhimu katika kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unakuwa huru na wa haki.

Miongoni mwa masuala aliyoyataja ni kuchelewa kwa IEBC kupata mfumo mpya wa usimamizi wa uchaguzi baada ya mkataba wa mfumo uliokuwa ukitumika awali kukamilika. Amesema kuchelewa kwa ununuzi wa mfumo huo kunaweza kuathiri zoezi la kuwasajili wapiga kura wapya pamoja na ukaguzi wa sajili ya wapiga kura.

Aidha, Gachagua amekosoa uongozi wa mwenyekiti wa IEBC, Erastus Edung Ethekon, akimtuhumu kukosa msimamo huru na kudai kuwa anapokea maagizo kutoka kwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama wa Ndani. Amemtaka mwenyekiti huyo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria badala ya kuingilia masuala ya kisiasa.

Kiongozi huyo wa DCP pia amesema upinzani utasukuma mabadiliko yatakayohakikisha kura zinahesabiwa na kutangazwa katika maeneo bunge, huku matokeo yatakayotangazwa yakichukuliwa kuwa ya mwisho.

Vilevile, amedai kuwa zoezi la usajili wa wapiga kura wapya linapewa kipaumbele katika maeneo yanayodhaniwa kuunga mkono serikali huku maeneo yanayohusishwa na upinzani yakiachwa nyuma.

Akizungumza wakati wa ibada ya kanisa la Wonders of God mjini Runyenjes, Kaunti ya Embu, Gachagua pia amepuuzilia mbali kauli ya serikali ya 'Usawa ni Sawa', akimtuhumu Rais William Ruto kuendeleza siasa zinazowagawa Wakenya.

Amesema serikali ya sasa imepuuza eneo la Mlima Kenya licha ya kujitokeza hadharani kuzungumzia usawa na ugavi wa rasilimali za taifa.

Katika ziara hiyo, Gachagua pia ameishutumu serikali kwa kuruhusu kuenea kwa pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya, akisema alikuwa amechukua hatua kukabiliana na tatizo hilo alipokuwa Naibu Rais.

Kuhusu siasa za vyama, Gachagua amewakaribisha viongozi wanaohama kutoka chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga na DCP, akisema chama chake kiko tayari kupokea viongozi wote wanaotaka kujiunga nacho.

Baadhi ya viongozi waliojiunga na chama hicho wamesema wamefika nyumbani kisiasa na kuahidi kumuunga mkono Gachagua katika azma yake ya kuwania urais.

Gachagua pia alitembelea maeneo ya Karurumo, mjini Runyenjes na soko la Kianjokoma, ambako alikutana na wakazi wakati wa ziara yake katika Kaunti ya Embu.