Shirikisho la Soka la Kimataifa,FIFA limeonya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) dhidi ya kuendesha mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Kitaifa (NEC) uliopangwa kufanyika Jumatano, Novemba 4, 2026.
Aidha linadai mkutano huo haukidhi matakwa ya katiba ya shirikisho hilo.
Katika barua rasmi iliyotumwa kwa FKF, FIFA imeeleza kuwa utaratibu uliotumika kuitisha mkutano huo unazua maswali kuhusu uhalali wake, hasa kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika Ibara ya 38 ya Katiba ya FKF.
FIFA imesema kuwa baada ya kupitia nyaraka na maelezo yaliyowasilishwa kuhusu kuitishwa kwa mkutano huo, imebaini kuwa msingi wa kisheria uliotumika huenda usiwe halali tena.
Kwa mujibu wa FIFA, mkutano huo uliitishwa Oktoba 27, 2026, ukiegemea ombi lililowasilishwa Mei 26, 2026, na baadhi ya wanachama wa NEC.
Hata hivyo, FIFA imebainisha kuwa baada ya ombi hilo kuwasilishwa, FKF iliitisha mkutano mwingine wa NEC Julai 11, 2026, na baadaye kutoa matangazo ya mikutano mingine ya kamati hiyo.
FIFA pia imeeleza kuwa wawili kati ya wanachama waliotia saini ombi la awali wamejiondoa rasmi na kuondoa uungwaji mkono wao kwa ombi hilo.
Kutokana na mabadiliko hayo, FIFA imesema ombi la Mei 26 haliwezi tena kutumika kama msingi halali wa kuitisha mkutano wa Novemba 4.
Shirika hilo la soka duniani limeongeza kuwa masharti yanayowaruhusu wanachama wa NEC kuitisha mkutano wao wenyewe chini ya Ibara ya 38.2 ya Katiba ya FKF hayajaonekana kutimizwa.
Katika hatua hiyo, FIFA imeiomba FKF kujizuia kuendesha mkutano huo uliopangwa kufanyika Novemba 4, ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu katiba na kuhakikisha vyombo vya kisheria vya shirikisho vinafanya kazi kwa utaratibu unaotakiwa.
Aidha, FIFA imeonya kuwa mikutano yoyote ya NEC itakayopangwa baadaye lazima iitishwe kwa kuzingatia kikamilifu masharti ya Katiba ya FKF, hususan Ibara ya 38 inayosimamia kuitishwa na kuendeshwa kwa mikutano ya kamati hiyo.
Barua hiyo inaweka shinikizo zaidi kwa uongozi wa FKF katika kipindi ambacho masuala ya utawala na uendeshaji wa shirikisho yanaendelea kuvuta hisia za wadau wa soka nchini.
Hatua ya FIFA inatarajiwa kuwa na athari kwa mipango ya NEC, huku ikisisitiza kuwa maamuzi ya kiutawala ndani ya shirikisho yanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa kikatiba ili kuepusha migogoro na kuhakikisha utulivu katika usimamizi wa soka la Kenya.
FIFA imehitimisha barua hiyo kwa kutaka FKF izingatie maelekezo hayo na kuchukua hatua zinazohitajika kuhakikisha mikutano ya NEC inafanyika kwa mujibu wa katiba.









