Familia moja mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta, imeomba msaada wa Wakenya ili iweze kupata mwili wa jamaa yao aliyefariki wakati akipokea matibabu mjini Eldoret, ambao umezuiliwa katika mochari kutokana na deni la hospitali.
Familia hiyo inasema imekumbwa na wakati mgumu tangu kufariki kwa George Mwawana Mwashumbe mwezi uliopita, baada ya kuugua kwa takribani miaka mitatu kutokana na maradhi ya ubongo yaliyohitaji matibabu ya muda mrefu.
Kwa mujibu wa mamake marehemu, Joyce Gombe, familia ilijitahidi kumtafutia mwanawe matibabu kwa miaka hiyo yote, huku juhudi hizo zikimfikisha katika hospitali moja mjini Eldoret kwa matumaini ya kupata huduma ambazo zingemsaidia kurejesha afya yake.
Hata hivyo, juhudi hizo hazikufanikiwa baada ya Mwawana kufariki dunia, na familia kujikuta katika changamoto nyingine ya kupata mwili wake ili kuandaa mazishi.
Gombe anasema mwili wa mwanawe umeendelea kuhifadhiwa katika mochari mjini Eldoret kutokana na familia kushindwa kulipa deni la matibabu, hali iliyovuruga mipango ya kumzika kwa heshima.
Nduguye marehemu, Dickson Mwandigha, amesema familia imejaribu kutafuta msaada kutoka kwa watu mbalimbali ili kukusanya fedha zinazohitajika, lakini juhudi hizo hazijazaa matunda.
Amesema kwa sasa familia imebaki na matumaini ya kupata msaada kutoka kwa Wakenya wenye moyo wa kujitolea huku wakiendelea kumwomba Mungu awavushe katika kipindi hicho kigumu.
Kisa hicho kinaibua tena mjadala kuhusu hospitali kuzuilia miili ya marehemu kutokana na madeni ya matibabu, licha ya msimamo wa mamlaka za afya kwamba miili ya watu waliofariki haipaswi kutumiwa kama dhamana ya kulipia huduma walizopokea.
Baraza la Madaktari na Madaktari wa Meno nchini (KMPDC) lilitoa ushauri kwamba hospitali zinapaswa kufanya makubaliano ya malipo na familia badala ya kuzuilia miili ya marehemu, likisisitiza kuwa haki ya utu inaendelea kuheshimiwa hata baada ya kifo.
Aidha, Bunge la Kitaifa lilipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Afya Novemba 11, 2026, unaopendekeza kudhibiti hospitali kuwazuilia wagonjwa waliotakiwa kuruhusiwa kutoka au miili ya marehemu kwa sababu ya madeni au bili.
Muswada huo unapendekeza pia hospitali kutumia hati za makubaliano ya kulipa madeni badala ya kuwazuilia marehemu, huku ukiweka adhabu kwa watakaokiuka masharti hayo.
Hata hivyo, familia ya Mwawana bado inakabiliwa na changamoto ya kupata mwili wake ili kumpa mazishi ya heshima.









