Seneta wa Trans Nzoia, Allan Chesang, ameitaka Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) pamoja na vyombo vya usalama kuanzisha uchunguzi kuhusu ongezeko la mvutano wa kisiasa na kikabila katika kaunti hiyo, akionya kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha amani na shughuli za kiuchumi.

Chesang amemkosoa Gavana George Natembeya kwa kile alichokitaja kuwa matamshi ya uchochezi, akidai kuwa baadhi ya kauli zake zimechangia kuongeza mgawanyiko miongoni mwa jamii zinazoishi katika kaunti hiyo.

Seneta huyo pia amemtuhumu gavana huyo kwa kutumia vijana na makundi anayoyataja kuwa wahuni kuwashambulia viongozi wengine kupitia mitandao ya kijamii, akitaka mamlaka husika kuchunguza madai hayo na kuwachukulia hatua wote watakaopatikana kuhusika.

Akizungumza kuhusu athari za mvutano huo, Chesang amesema hali ya sintofahamu ya kisiasa imeanza kuathiri mazingira ya biashara na uwekezaji, akionya kuwa wawekezaji wanaweza kukwepa eneo hilo iwapo usalama na utulivu hautahakikishwa.

Trans Nzoia ni miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa chakula nchini, hivyo kwa mujibu wa seneta huyo, kuendelea kwa mivutano kunaweza kuathiri shughuli za wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea kilimo kujipatia kipato.

Aidha, Chesang amelaani shambulio dhidi ya Amos Masika, mwanablogu na afisa wa mawasiliano katika ofisi ya Gavana Natembeya, akisema tukio hilo linaonyesha haja ya kuimarishwa kwa usalama wa viongozi na wananchi bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

Masika alishambuliwa na watu waliokuwa na mapanga nyumbani kwake usiku wa Novemba 16, 2026, katika eneo la Chebarus, Trans Nzoia, ambapo alipata majeraha makubwa kichwani, mikononi na miguuni huku gari lake likichomwa moto.

Tukio hilo limezua mjadala kuhusu usalama wa viongozi na wananchi katika eneo hilo. Kwa mujibu wa taarifa za polisi, washukiwa wanne walikamatwa kuhusiana na shambulio hilo na kuruhusiwa kuzuiliwa kwa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi.

Wasiwasi kuhusu uhusiano wa ukabila katika kaunti hiyo pia uliwahi kuibuliwa mwaka 2025, wakati mvutano kati ya gavana na naibu wake ulipoibua hofu ya kuongezeka kwa mgawanyiko kati ya jamii za Waluhya na Wakalenjin.

Chesang sasa anataka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha mvutano huo na kuhakikisha wanaohusika wanawajibishwa kabla hali haijazidi kuwa mbaya.