Serikali ya Canada imewaalika Wakenya na wataalamu wengine kutoka mataifa mbalimbali kutuma maombi ya kupata ukaazi wa kudumu nchini humo kupitia mpango wa uhamiaji wa wafanyakazi wenye ujuzi, huku taifa hilo likitafuta kukabiliana na uhaba wa wafanyakazi katika sekta muhimu za uchumi wake.

Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia nchini Canada (IRCC) imesema inahitaji wataalamu wenye ujuzi kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kuimarisha sekta zinazokabiliwa na upungufu wa wafanyakazi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Katika taarifa iliyochapishwa Ijumaa, Novemba 20, 2026, idara hiyo iliwahimiza watu wanaotaka kuhamia nchini humo kuanza kuandaa nyaraka zinazohitajika ili kujiunga na mfumo wa Express Entry unaosimamia maombi ya ukaazi wa kudumu.

Canada's immigration invitation for skilled workers

“Canada inatafuta wafanyakazi wenye ujuzi ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, kuimarisha sekta muhimu za uchumi na kukidhi mahitaji mbalimbali ya soko la ajira nchini kote,” ilisema IRCC.

Mpango wa Express Entry unaruhusu wataalamu wanaoishi nje ya Canada, wakiwemo Wakenya, kutuma maombi ya kuhamia nchini humo kwa misingi ya elimu, uzoefu wa kazi na uwezo wa lugha.

Sekta zinazotafutiwa wataalamu

Canada imeorodhesha sekta kadhaa zinazohitaji wafanyakazi wenye ujuzi, zikiwemo afya na huduma za kijamii, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Sekta nyingine ni elimu, usafiri na biashara za ufundi stadi kama vile umeme, uchomeleaji na ufundi wa magari.

Pia, wataalamu wanaozungumza Kifaransa wanaweza kuzingatiwa katika baadhi ya awamu za uteuzi, huku madaktari na watafiti wakiwa miongoni mwa makundi mengine yanayolengwa.

Hata hivyo, kufanya kazi katika mojawapo ya sekta hizo hakumaanishi mtu atapata moja kwa moja kibali cha makaazi wa kudumu.

Application process for residency

Jinsi ya kutuma maombi

Kupitia Express Entry, waombaji wanatakiwa kwanza kuunda akaunti na kuweka taarifa zao kuhusu elimu, uzoefu wa kazi, umri na uwezo wa kuzungumza Kiingereza au Kifaransa.

Waombaji wanaokidhi vigezo huingizwa katika orodha ya watahiniwa na kupewa alama kupitia mfumo wa Comprehensive Ranking System (CRS), unaotumika kupima uwezo wao ikilinganishwa na wengine.

Canada huandaa awamu za uteuzi na kuwaalika watahiniwa wenye alama za juu zaidi kutuma maombi rasmi ya kupata ukaazi wa kudumu.

Mfumo huo unasimamia programu tatu kuu ambazo ni Federal Skilled Worker Program, Federal Skilled Trades Program na Canadian Experience Class.

Nyaraka zinazohitajika

Required documents for application

IRCC imewahimiza wataalamu waliohitimu nje ya Canada kuhakikisha vyeti vyao vya elimu vinatathminiwa na taasisi zinazotambuliwa kupitia utaratibu wa Educational Credential Assessment (ECA), pale inapohitajika.

Aidha, wanapaswa kufanya mitihani ya lugha inayotambuliwa na Canada ili kuthibitisha uwezo wao wa kuwasiliana kwa Kiingereza au Kifaransa.

Nyaraka nyingine zinazoweza kuhitajika ni pasipoti, vyeti vya polisi, uthibitisho wa uzoefu wa kazi na ushahidi wa kuwa na fedha za kujikimu wanapowasili nchini humo.

Serikali ya Canada imesisitiza kuwa kutimiza masharti ya awali hakuhakikishi kupata ukaazi wa kudumu, kwani kila mwombaji atapimwa kulingana na vigezo vya programu husika.

Wakenya wanaotaka kuomba wameelekezwa kutumia tovuti rasmi ya idara ya uhamiaji ya Canada kupata maelekezo na kuwasilisha maombi yao.