Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ushirikiano na Kenya, Tanzania na Uganda limezindua rasmi nembo ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, itakayofanyika kwa pamoja katika mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki.
Nembo hiyo iliyozinduliwa Alhamisi, Novemba 19, 2026, katika nchi zote tatu wenyeji, imepewa jina la AFCON PAMOJA 2027, ikiwa ni sehemu ya utambulisho rasmi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni 19, 2027.
Kwa mujibu wa CAF, nembo hiyo imechochewa na ngao ya jadi ya Afrika Mashariki, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ishara ya utambulisho, ulinzi, fahari na umoja katika jamii za eneo hilo.
Uchaguzi wa ngao hiyo una umuhimu wa kipekee kwa mataifa hayo matatu kwa kuwa alama hiyo inapatikana pia katika nembo za taifa za Kenya, Tanzania na Uganda, ikiwakilisha historia na urithi unaofanana kati ya nchi hizo.
Katika muundo wa nembo hiyo, kombe la AFCON limewekwa katikati ya ngao, huku likiwa limezungukwa na mchoro wa bara la Afrika pamoja na jina la CAF.
Muundo huo pia umejumuisha mapambo ya rangi na michoro ya kijiometri inayotokana na sanaa za jadi za Afrika Mashariki, ikiwemo ushanga, ufumaji na utengenezaji wa vitambaa vya asili.
Rangi za mataifa yote matatu zimeunganishwa katika nembo hiyo. Rangi nyekundu na nyeusi zimewekwa sehemu ya juu, kijani na njano pembeni mwa kombe, huku bluu ikionekana sehemu ya chini.
Aidha, CAF imefichua kuwa utambulisho mpya wa mashindano hayo hautaishia kwenye nembo kuu pekee, bali utajumuisha michoro 12 tofauti ya ngao itakayoakisi utambulisho wa kila taifa mwenyeji.
Kwa upande wa Kenya, michoro hiyo itatumia mistari mipana ya mlalo inayoashiria nguvu, urithi na umiliki, huku Tanzania ikiwakilishwa na mistari ya mshazari inayotokana na bendera yake ya taifa.
Uganda nayo itatumia mchanganyiko wa rangi mbalimbali pamoja na picha ya ndege aina ya korongo mwenye taji, anayehusishwa na utambulisho wa taifa hilo.
CAF imesema utambulisho huo mpya utatumika katika viwanja, majukwaa ya kidijitali na shughuli mbalimbali za mashindano hayo ili kuonyesha utamaduni na urithi wa Afrika Mashariki kwa mashabiki wa soka duniani.
Neno PAMOJA, linalomaanisha kuwa pamoja, limechaguliwa kuwakilisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Kenya, Tanzania na Uganda katika kuandaa mashindano hayo.
Michuano hiyo itaanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027, huku ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya AFCON kwa mataifa matatu kuandaa mashindano hayo kwa pamoja.
CAF imesema zikiwa zimesalia siku 212 kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, uzinduzi wa nembo ni hatua muhimu katika maandalizi ya tukio hilo kubwa la soka barani Afrika. Confédération Africaine de Football









