Bunge la Kaunti ya Mombasa limeibua wasiwasi kuhusu hali ya kifedha ya serikali ya kaunti hiyo, kufuatia kushuka kwa mapato ya kawaida, kuongezeka kwa madeni ambayo hayajalipwa na matumizi duni ya fedha zilizotengewa miradi ya maendeleo.

Katika ripoti iliyopitishwa na bunge hilo, Kamati ya Fedha, Bajeti na Ugawaji wa Fedha imebainisha kuwa serikali ya kaunti ilishindwa kufikia malengo yake ya ukusanyaji wa mapato ya kawaida kwa shilingi bilioni 2.87, hali inayozua maswali kuhusu usimamizi wa rasilimali za kifedha.

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa madeni ambayo serikali ya kaunti inadaiwa na wadai mbalimbali yamefikia shilingi bilioni 2.95, huku baadhi ya malipo hayo yakidaiwa kukwama kwa zaidi ya miaka mitatu bila kutatuliwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Swaleh Kibwana Baya, amesema kiwango cha matumizi ya fedha za maendeleo pia kimekuwa cha chini, huku ni asilimia 45.8 pekee ya bajeti iliyotengewa miradi ya maendeleo iliyotumika katika kipindi kilichokaguliwa.

Kutokana na hali hiyo, kamati imeitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwasilisha orodha kamili na iliyothibitishwa ya madeni yote ambayo hayajalipwa, ikiambatana na mpango madhubuti wa kuhakikisha wadai wanalipwa.

Kamati hiyo imesisitiza umuhimu wa serikali kuweka wazi muda ambao itachukua kulipa madeni hayo, ikionya kuwa kucheleweshwa kwa malipo kunaweza kuathiri utekelezaji wa shughuli za kibiashara pamoja na utoaji wa huduma kwa wakazi wa kaunti hiyo.

Aidha, serikali ya kaunti imeagizwa kutoa maelezo ya kina kuhusu miradi ya maendeleo ambayo imesimama au kuchelewa kukamilika, huku ikishauriwa kuelekeza rasilimali zilizopo katika kukamilisha miradi hiyo badala ya kuanzisha mingine mipya.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, kuanzisha miradi mipya wakati ile ya awali haijakamilika kunaweza kuongeza mzigo wa kifedha kwa serikali ya kaunti na kuchelewesha zaidi utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Wakati huo huo, kamati imeonya kuwa mahitaji ya miradi iliyopendekezwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028 yanazidi kiwango cha fedha zinazopatikana, hali inayohitaji serikali kufanya tathmini upya ya vipaumbele vyake.

Aidha,kamati imeitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha miradi inayopangwa inaendana na uwezo wake halisi wa kifedha ili kuepusha kuongezeka kwa madeni na miradi kukwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Kamati imesisitiza kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na ukusanyaji bora wa mapato ni muhimu katika kuhakikisha wakazi wa Mombasa wanapata huduma bora na miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.