Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ametangaza azma ya kubadilisha sura ya Jiji la Nairobi iwapo atapata nafasi ya kuliongoza, akiahidi kukabiliana na changamoto za uchafu, barabara mbovu na usumbufu unaowakabili wafanyabiashara kutoka kwa maafisa wa kaunti maarufu kama Kanjo.

Babu, ambaye ni kiongozi wa chama cha The Mwananchi Party (TMP), alitoa ahadi hizo wakati wa ziara ya chama hicho jijini Nairobi, ambapo alieleza kuwa ana mipango ya kuleta mabadiliko katika uongozi na utoaji wa huduma kwa wakazi wa jiji hilo.

Akizungumza na wakazi na wafuasi wake, mwanasiasa huyo alisema Nairobi inahitaji uongozi unaoelewa changamoto za wananchi wa kawaida, hasa wafanyabiashara wadogo wanaotegemea shughuli zao za kila siku kujipatia riziki.

Aliahidi kuwa serikali atakayoiongoza itakomesha vitendo vya kuwanyanyasa wafanyabiashara kupitia operesheni za maafisa wa Kanjo, akisema wafanyabiashara wanapaswa kupewa mazingira mazuri ya kufanya biashara badala ya kuishi kwa hofu ya kukamatwa au kusumbuliwa.

"Nitakomesha mambo ya Kanjo kuwahangaisha wafanyabiashara. Wananchi wanapaswa kufanya biashara zao kwa amani na kupata riziki bila usumbufu," alisema.

Kuhusu elimu, Babu aliahidi kuanzisha mfumo wa utoaji wa bursari utakaohakikisha watoto kutoka familia zenye mahitaji wanapata nafasi ya kuendelea na masomo bila ubaguzi wa kisiasa, kikabila au kijamii.

Alisema hakuna mtoto anayepaswa kunyimwa nafasi ya kupata elimu kutokana na hali ya kifedha ya familia yake au uhusiano wa wazazi wake na viongozi wa kisiasa.

Aidha, mbunge huyo alijigamba kuwa amekuwa akiorodheshwa miongoni mwa wabunge wanaofanya vizuri zaidi nchini, akisema uzoefu wake katika kuongoza Embakasi Mashariki utakuwa msingi wa kuleta mageuzi Nairobi.

Alisema analenga kuimarisha miundombinu ya barabara, kuboresha usafi wa mazingira na kuhakikisha wakazi wanapata huduma bora.

Katika ujumbe wake wa kisiasa, Babu alisema maeneo mbalimbali nchini tayari yana vyama vinavyotambulika kisiasa, akitaja Nyanza, eneo la Kati, Bonde la Ufa, Pwani na Magharibi.

Alisema Nairobi nayo inapaswa kuwa na chama chake, akiwataka wakazi kukumbatia The Mwananchi Party kama chombo cha kuwakilisha maslahi yao.

"Hapa Nairobi chama chetu ni TMP," alisema Babu, akihimiza wakazi kuunga mkono ajenda ya chama hicho katika safari yake ya kisiasa.