Washukiwa watano wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya wakili maarufu Mathew Kyalo Mbobu wamekanusha kuhusika na kifo chake, huku upande wa mashtaka ukidokeza kuwa huenda mtu mwingine akaunganishwa na kesi hiyo.

Washukiwa hao walifikishwa mbele ya Jaji Diana Kavedza katika Mahakama Kuu ya Kibera jijini Nairobi Jumanne, Oktoba 27, 2026, ambapo kila mmoja alikana shtaka la mauaji.

Washukiwa hao ni Rose Mbithe Mulwa, watoto wake Chris Mulwa na Angela Mulwa, pamoja na maafisa wawili wa polisi, Julius Kipkoech Cheruiyot na Kennedy Kipkemoi Borboroi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watano hao wanadaiwa kumuua Mbobu mnamo Septemba 9, 2025, kando ya Barabara ya Magadi, karibu na Shule ya Brookhouse International katika eneo la Karen, kaunti ya Nairobi.

Upande wa mashtaka unadai kuwa washukiwa hao walitenda kosa hilo kwa pamoja na watu wengine ambao bado hawajafikishwa mahakamani.

Mbobu, ambaye alikuwa wakili mashuhuri wa Mahakama Kuu, mhadhiri wa chuo kikuu na mwandishi, aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akisafiri kuelekea nyumbani kutoka kazini.

Uchunguzi wa mwili wake ulionyesha kuwa alikuwa na majeraha manane ya risasi katika sehemu za kidevu, shingo na kifua, yaliyosababisha kuvuja damu nyingi na kifo chake.

Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu kutokana na mazingira ya mauaji hayo na madai ya uwezekano wa watu kadhaa kuhusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huo.

Katika hatua nyingine, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuhusu nia yake ya kumfungulia mashtaka Inspekta wa Polisi Kenneth Kipkemboi Sang kuhusiana na mauaji ya Mbobu.

Sang alikamatwa Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, mwishoni mwa wiki na baadaye kufikishwa katika Mahakama za Milimani, Nairobi, ambako mahakama iliidhinisha kuzuiliwa kwake kwa siku 14 ili kuwapa wachunguzi muda wa kukamilisha uchunguzi.

Maafisa wa upelelezi wanachunguza madai ya kuhusika kwake katika mauaji ya Mbobu na yale ya Dkt Victoria Nthunya Mutiso, mwanasaikolojia aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Upper Hill, Nairobi, Julai 29, 2026.

Kufunguliwa kwa kesi ya mauaji ya Mbobu kunaongeza changamoto za kisheria kwa Rose Mbithe na watoto wake wawili, ambao pia wanakabiliwa na mashtaka tofauti ya mauaji ya Dkt Mutiso.

Kuhusu suala la dhamana, upande wa mashtaka umeeleza kuwa unapinga kuachiliwa kwa washukiwa hao kwa dhamana wakati kesi ikiendelea.

Wakili wa upande wa utetezi, Joel Mbaluka, alikuwa ameeleza kuwa washukiwa walitaka kuwasilisha maombi ya dhamana kwa njia ya mdomo.

Hata hivyo, Jaji Kavedza alielekeza kuwa maombi hayo yawasilishwe rasmi kwa maandishi.

Mahakama imeagiza upande wa utetezi kuwasilisha maombi na hoja zake ndani ya siku 10, huku maafisa wa uangalizi wa jamii wakitakiwa kuwahoji washukiwa na familia za waathiriwa ili kuandaa ripoti zitakazosaidia mahakama kuamua kuhusu dhamana.

Usikilizaji wa maombi ya dhamana umepangwa kufanyika Novemba 24, 2026, huku kesi ikitajwa tena Novemba 19, 2026, ili kufuatilia hatua zilizochukuliwa na pande husika.

Washukiwa hao wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi pale mahakama itakapothibitisha vinginevyo.