Naibu Rais wa Kenya,Kithure Kindiki amewaonya wakazi wa eneo la Mlima Kenya dhidi ya kujihusisha na siasa za kikabila.
Aidha amewataka viongozi kuzingatia ajenda za maendeleo badala ya kutumia tofauti za kisiasa kugawanya wananchi.
Kindiki anasema ushindani wa kisiasa haupaswi kuwa sababu ya kuchochea chuki, mizozo au uhasama kati ya jamii, akisisitiza kuwa Wakenya wanapaswa kuheshimiana licha ya kuwa na misimamo tofauti kuhusu uchaguzi na uongozi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Nessuit, kaunti ya Nakuru, Jumanne, Oktoba 27, 2026, Naibu rais aliwataka wanasiasa wanaotafuta uungwaji mkono kueleza rekodi zao za maendeleo na mipango waliyo nayo ya kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema viongozi wanapaswa kushindana kwa sera na mawazo yanayoweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi badala ya kutumia matusi, majina ya kejeli na matamshi yanayoweza kuchochea migawanyiko.
Kindiki pia aliwataka wakazi kuruhusu wanasiasa wenye misimamo tofauti kueleza sera zao kwa amani, akionya dhidi ya vitendo vya vurugu, vitisho na uharibifu wa mali wakati wa mikutano ya kisiasa.
Alisisitiza kuwa kila Mkenya ana haki ya kushiriki katika shughuli za kisiasa bila kutishwa au kushambuliwa kwa sababu ya msimamo wake.
Naibu Rais alisema serikali inalenga kuhakikisha fursa za maendeleo zinagawanywa kwa usawa bila kujali kabila, dini, umri au eneo ambalo mtu anatoka.
Alitetea sera za kiuchumi za serikali ya Kenya Kwanza, akisema zinapaswa kuwanufaisha wananchi wa kawaida wakiwemo wakulima, wafanyabiashara wadogo na watu wanaojitafutia riziki katika maeneo ya mashinani.
Katika kuonyesha juhudi za serikali katika sekta ya maendeleo, Kindiki alitaja miradi ya barabara, usambazaji wa umeme na ujenzi wa masoko ya kisasa katika kaunti ya Nakuru.
Alisema serikali imeweka kipaumbele katika ujenzi wa kilomita 870 za barabara katika kaunti hiyo kwa gharama ya Sh38 bilioni, huku miradi ya umeme yenye thamani ya Sh3 bilioni ikilenga kuunganisha kaya 25,000 zaidi.
Katika eneo bunge la Njoro, Kindiki alisema Sh370 milioni zimetengwa kuunganisha kaya nyingine 3,200 na huduma ya umeme.
Pia alitaja ujenzi wa masoko ya kisasa katika maeneo ya Nessuit, Mauche na Kihingo, akisema miradi hiyo inalenga kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara.
Kauli za Kindiki zinajiri wakati shughuli za kisiasa zikishika kasi nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku viongozi mbalimbali wakijipanga kutafuta uungwaji mkono katika maeneo tofauti.
Naibu Rais aliwataka wakazi kutathmini viongozi kwa kuzingatia kazi walizofanya na mipango yao ya maendeleo, akisisitiza kuwa umoja wa taifa unapaswa kutangulizwa kuliko tofauti za kisiasa.
Alisema ushindani wa uchaguzi unapaswa kuwa njia ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka badala ya kuwa chanzo cha uhasama unaoweza kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.









