Viongozi wa kijeshi nchini Guinea-Bissau wameahirisha uchaguzi wa rais na wabunge uliokuwa umepangwa kufanyika Desemba 6, 2026, na kuusogeza hadi Novemba 2028, hatua inayochelewesha kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo.
Uamuzi huo umetangazwa kupitia amri iliyotolewa Alhamisi na Rais wa mpito, Meja Jenerali Horta Inta-a, ambaye alisema uchaguzi huo hautafanyika kwa wakati uliokuwa umepangwa kutokana na ukosefu wa mazingira muhimu ya kuandaa zoezi hilo.
Katika amri hiyo, serikali ya kijeshi imesema kuwa kuna upungufu wa rasilimali za kiufundi, vifaa na fedha zinazohitajika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia inayokidhi viwango vinavyotakiwa.
Viongozi hao wamedai kuwa kufanya uchaguzi bila kukamilisha maandalizi muhimu kunaweza kuathiri uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na imani ya umma katika mchakato wa uchaguzi.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa utawala wa kijeshi utaendelea kuongoza taifa hilo la Afrika Magharibi kwa takribani miaka miwili zaidi, licha ya ahadi ya awali ya kurejesha utawala wa kiraia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya mapinduzi.
Jeshi lilitwaa mamlaka Novemba 26, 2025, siku tatu baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, na kusitisha mchakato wa uchaguzi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.
Wakati huo, Rais wa zamani Umaro Sissoco Embaló, aliyekuwa akitafuta muhula mwingine, pamoja na mpinzani wake mkuu Fernando Dias, walikuwa wametangaza madai ya ushindi.
Baada ya mapinduzi hayo, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Horta Inta-a, aliapishwa kuwa kiongozi wa mpito na kupewa jukumu la kusimamia kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi na kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Hata hivyo, mkataba wa mpito uliotangazwa na utawala wa kijeshi ulimzuia Inta-a kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao.
Mwezi Oktoba mwaka huu, Waziri Mkuu wa mpito Ilídio Vieira Té alikuwa amesema kuwa mazingira hayakuwa tayari kwa uchaguzi wa Desemba, ingawa hakutangaza tarehe mpya ya kufanyika kwa zoezi hilo.
Uamuzi huo pia unakuja miezi kadhaa baada ya wananchi kupitisha mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maoni mwezi Agosti, mabadiliko yaliyoongeza mamlaka ya rais.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ilikuwa imeitaka Guinea-Bissau kuhakikisha inarejea katika utawala wa kikatiba kupitia kipindi kifupi, kilichopangwa kwa uwazi na kuwahusisha wadau mbalimbali.
Guinea-Bissau, yenye wakazi takribani milioni 2.2, imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa, mapinduzi na majaribio ya mapinduzi tangu ilipopata uhuru kutoka Ureno zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Taifa hilo pia linatajwa kuwa njia muhimu ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka Amerika Kusini kuelekea Ulaya, hali ambayo wataalamu wanasema imechangia changamoto zake za kisiasa.









